Karibu

Karibu kwenye tovuti ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Baraza hili  lilianzishwa mwaka 2005 ili kutekeleza maagizo yaliyomo kwenye Sera ya Taifa ya Uwezeshaji ya mwaka 2004. Mwaka huo huo Sheria ya Uwezeshaji ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kutia mkazo zaidi katika utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji.  Katika tovuti hii kuna taarifa mbalimbali kuhusu Baraza, majukumu, nguzo na fursa za Uwezeshaji, maeneo ya ushirikiano na pia kuna anuwani ya tovuti za washirika. Kitendo cha wewe kutembelea tovuti yetu tunakijali sana na tuna karibisha maswali, mawazo na ushauri wako.

Utangulizi

Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iliundwa mwaka 2004 na mwaka huo huo sheria ya Uwezeshaji na.16 ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili majukumu ya Sera yaweze kutekelezwa kisheria. Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ilianzishwa kwa ibara ya Nne (4) ya sheria ya Uwezeshaji. Baraza lilianzishwa rasmi mwaka 2005 likiwa ni chombo cha juu cha kusimamia utekelezaji wa sera ya ya Taifa ya Uwezeshaji.

Baada ya Uhuru Tanzania iliandaa Sera na mikakati mbalimbali  ikiwa na lengo la kuendeleza nchi kwa ujumla na kuwawezesha wananchi kushiriki katika kujenga uchumi wa nchi yao. Sera na mikakati iliyobuniwa ni pamoja na Azimio la Arusha, Madaraka Mikoanai, Mageuzi ya kibiashara na ubinafsishaji wa mashirika ya umma. Ingawa Sera na mikakati iliyobuniwa haikuwa na mafanikio mazuri katika nyanja za uchumi, ilijenga msingi madhubuti ya amani, upendo na umoja wa kitaifa ambavyo ndiyo nyenzo za maendeleo ya kiuchumi.

Dira

Imani yetu ni kuwa Baraza hili litakuwa kiongozi katika kuwezesha, kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Dhima

 Kuwaongoza watanzania katika kujenga uchumi wenye nguvu kwa kuboresha mazingira ya kibiashara na kutoa fursa sawa za kiuchumi.

Baraza linatoa huduma zake kwa kuzingatia:

 1. Uwazi
 2. Haki
 3. Usikivu
 4. Uwezo
 5. Kuwajibika
 6. Umoja
 7. Kujitoa

Madhumuni

 1. Kutoa mwongozo utakaosaidia Watanzania walio wengi kupata fursa sawa za kumiliki uchumi na;
 2. Kutoa upendeleo maalum kwa Watanzania (inapobidi) ili kuwawezesha kujenga uwezo pamoja na kunufaika na fursa za kiuchumi zilizopo.

Kazi za Msingi za baraza

 1. Kuandaa Mpango Mkakati wa sekta na kisekta na kuhamasisha matumizi ya rasilimali kwa shughuli za Uwezeshaji Kiuchumi;
 2. Kuhamasisha na kuhimiza uwekaji wa akiba, uwekezaji, na ushirikishwaji makini wa wananchi kwenye shughuli za kiuchumi;  
 3. Kusimamia, kuongoza na kubaini vyanzo vya fedha kwa ajili ya mfuko wa udhamini;
 4. Kuwezesha na kuratibu Uwezeshaji na mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi mbalimbali vya Wananchi kutegemeana na mahitaji yao na changamoto zao;
 5. Kushirikiana na mashirika mbalimbali kwa nia ya kuhamasisha Uwezeshaji na upatikanaji wa huduma zinazohusiana na fursa za kiuchumi;
 6. Kuhamasisha utafiti wa shughuli za kiuchumi na kuhimiza ushirikiano na masirika ya utafiti; na
 7. Kuandaa mfumo wa kufuatilia maendeleo ya shughuli za kiuchumi na mfumo wa menejimenti wa habari za uwezeshaji;

Ili kusoma machapisho ya kiswahili bonyeza hapa.