Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limetenga kiasi cha shilingi bilioni moja za kitanzania kwa ajili ya kudhamini mikopo inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa Vyama vya Ushirika na Akiba na Mikopo cha Waendesha Bodaboda Nchini.

Mkopo huo unalenga kuwawezesha vyama vya kuweka na kukopa nchini vitakavyoanzishwa na waendesha bodaboda wote  na kwa kuanzia na Chama cha Ushirika na Akiba na Mikopo Waendesha Boda Boda  Dar es Salaam (DABOSA) ili waweze kukua,kuinuka kimtaji na kumiliki bodaboda zao kwa kuwa wengi wameajiriwa kuendesha bodaboda hizo.

Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Beng’i Issa alisema hayo mara baada ya kutiliana saini ya makubaliano ya kudhamini Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutoa mikopo DABOSA ili iweze kutoa mikopo kwa wanachama wake.

“Fedha hizI za kudhamini mikopo hii zitawekwa kwenye akaunti ya mfuko huo na wao wametenga shilingi tatu kwa ajili ya kazi hiyo” alisema na kuongeza kuwa watatoa mkopo kwa riba ya asilimia 9.32 na DABOSA itatoza kwa wanachama wake kwa asilimia 12.3.

Alifafanua zaidi, Bi. Issa alisema mpango huo ni wa kitaifa wenye lengo la kuwezesha wananchi kiuchumi, hiyo watashirikiana na mfuko huo kuwapatia mafunzo ya utawala bora, kuweka akiba na ujasirimali.

“Mafunzo yameshaanza kutolewa Dar es Salaam na yataendelea kufanyika pia katika mikoa mingine nchini,” alisisitiza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dkt. Ramadhani Dau alisema mikopo hiyo ni njia ya kuwezesha vijana kuondokana na tatizo la ajira ambalo linawakabili.

“Mfuko umejiweka tayari kutoa mikopo hii, lakini jambo la msingi ni kwa vijana waweze kufanya kazi kwa bidii,na kuwa waaminifu katika biashara zao ili waweze kurejesha mikopo,”alisema Dkt. Dau.

Mkurugenzi huyo Mkuu aliwaelezea waendesha bodaboda hao kuwa mfuko unatoa huduma za jamii zikiwemo za mafao ya ajali na mafao ya afya, hivyo wanaweza kujiunga na kunufaika nayo wakati wanaendelea na shughuli zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji,Bw. Omari Issa ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais Utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),alisema programu ya kuwezesha bodaboda ni moja ya mambo ambayo yaliyomo katika BRN.

“Baraza limeondokana na mfumo wa zamani wa kutoa mikopo kwa wananchi moja kwa moja na sasa inadhamini taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wananchi,” alisema.

Alisema wanafanya hivyo na Benki ya Posta, TIB, NSSF na  watashirikiana na taasisi zingine ili kuendelea kuwafikiwa wananchi wengi zaidi.

Mwenyekiti wa DABOSA,Bw. Said Kagomba alisema chama chao ni cha vijana wa jiji la Dar es Salaam kina wanachama 439; Kinondoni (135),Ilala (163) na Temeke (141).

“Lengo ni kuinua,kustawisha na kuboresha hali ya maisha yetu” na mpaka sasa wamekusanya kiasi cha shilling milioni 24.7,”alisema Bw.Kagomba.

Chama kinatarajia kuanza kutoa mikopo kwa wananchama wake kuanzia sasa ambapo utiaji wa saini kati ya Baraza  na NSSF umekamilika.