Habari

Imewekwa: Aug, 13 2019

Elimu ya mikopo na ruzuku yawagusa vijana Dodoma

News Images

VIJANA wanaoshiriki mafunzo ya ujasiriamali na kuboresha biashara yanayoendelea kufanyika Mjini Dodoma wamefurahishwa na ushiriki wa wakufunzi kutoka kwenye Mifuko ya Uwezeshaji ambao wanatoa elimu za fursa za mikopo na ruzuku.

Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji wanaendesha mafunzo hayo ambayo yamepangwa kuwafikia vijana wasiopungua 4000 kutoka katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.

Mafunzo haya ambayo yameshirikisha taasisi za urasimishaji wa biashara, Taasisi za fedha na Mifuko ya Uwezeshaji yamelenga kuboresha biashara za vijana na kupanua wigo wa ajira kwa Watanzania wote.

Akizungumza na Afisa Habari wa Baraza la Uwezeshaji Mjasiriamali Martha Simon ambaye ni mmiliki wa Saluni ya kike amesema kuwa uwepo wa Mifuko ya Uwezeshaji imesaidia kupanua uelewa juu ya njia wanazopaswa kupita ili wanufaike na fursa za mikopo na ruzuku zinazotolewa na Serikali.

“Tumepita katika mafunzo mengi ya ujasiriamali lakini haya ya sasa yapo tofauti kutokana na uwepo wa wakufunzi wanaotoka moja kwa moja kwenye taasisi husika za masuala ya mikopo na ruzuku,”alisema Martha.

“Tumeyapokea vizuri mafunzo haya kwani hapo mwanzo tulikuwa na hofu ya kuzisogelea fursa za mikopo kutoka kwenye mifuko lakini sasa kila mshiriki amepata mwanga baada kwa kuelewa dhana nzima ya uwezeshaji na hatua anazopaswa kupita ili anufaike na fursa zilizopo aliongeza Mjasiriamali huyo.

Mafunzo haya yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista Mhagama (MB) katika ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.

Awamu ya pili ya Mafunzo haya inatarajia kufanyika kwenye mji wa Songea yakishirikisha vijana kutoka kada mbalimbali za uzalishajimali.