Habari

Imewekwa: Jun, 17 2021

​MAHAFALI YA KWANZA YA VIJANA WAJASIRIAMALI CHINI YA PROGRAMU YA KCB 2JIAJIRI

News Images

Mahafali hayo yamefanyika leo katika ukumbi wa Protea Hotel Jijini Dar es Salaam yakisimamiwa na Benki ya KCB ambao ndio waandaaji wa mafunzo haya ya Ujasiriamali yanayofanyika chini ya Programu maalum ya KCB 2jiajiri.

Akimwakilisha Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji, Bw. Gwakisa Bapala (Meneja wa Mipango na Tafiti - NEEC) alitoa pongezi kwa Benki ya KCB kwa kufanikisha awamu hiyo ya mafunzo iliyowagusa moja kwa moja vijana wapatao 118 wa Kitanzania waliopata mafunzo kutoka Chuo cha VETA.

"Naomba kuchukua fursa hii kuwapongeza Benki ya KCB kwa kuwafikiria Vijana na kuanzisha programu hii na nawaomba vijana muone fursa hii kama bahati na kuitumia ipasavyo kuboresha maisha yenu" alisema Bw. Gwakisa

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji KCB Bw. Pascal Machango alisema programu ya mafunzo haya ni endelevu tunaishukuru Serikali kupitia Baraza la Uwezeshaji kwa kuiona juhudi yetu hivyo tutashirikiana bega kwa bega katika kuwawezesha vijana kiuchumi.

"Kwa dhati kabisa nawaomba Vijana mnaohitimu leo mkawe mabalozi kwa wengine, mkawasaidie Vijana wengine, mkawashike mkono na kuwaonesha njia sahihi" alisisitiza Bw. Pascal

Kwa upande wake Mratibu wa Programu hii kutoka Benki ya KCB Bi. Christina Manyenye amesema lengo kuu la Mafunzo haya ni kubadilisha mtazamo wa Vijana kutoka kwenye dhana ya kuajiriwa kwenda katika dhana ya kujiajiri, hii itawasaidia Vijana wengi kwani wataajiri vijana wengine wengi zaidi kupitia shughuli zao.

"Tunaomba mkayafanyie kazi mafunzo haya ambayo mnahitimu leo, mmetuonesha juhudi na juhudi hiyohiyo muendelee nayo" aliongezea Bi. Christina

Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Eng. Joseph Mwanda ameishukuru Benki ya KCB kwa ushirikiano wao walioutoa tangu mwanzo wa mafunzo mpaka siku hii ya Mahafali na amewakaribisha tena katika awamu nyingine ya mafunzo.