Habari

Imewekwa: Oct, 06 2021

MHE. MWAMBE ALITAKA BARAZA LA UWEZESHAJI KUFANYA UTAFITI WA KUTOSHA ILI KUONGEZA UFANISI KIUTENDAJI

News Images

Hayo yameelezwa wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Uwezeshaji na Maendeleo ya sekta binafsi Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) alipotembelea Ofisi za Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa lengo la kuzungumza na Bodi ya Baraza pamoja na Menejimenti ya Baraza.

Katika ziara yake hiyo Mhe. Waziri aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Uwezeshaji na maendeleo ya sekta binafsi Prof. Godius W. Kahyarara na watumishi wengine kutoka Idara ya Uwezeshaji.

Mhe. Mwambe amelitaka Baraza kufanya tafiti kuhusiana na suala la mitaji na masuala ya riba hali ambayo itasaidia kuonyesha namna mitaji inavyoweza kupatikana, athari za riba kubwa na njia za kusaidia kuzipunguza kama namna ya kuwawezesha Watanzania.

Aliongeza kuwa sera ya uwezeshaji ni mtambuka na inamhusu kila mtu na sekta zote hivyo kuna umuhimu wa Baraza kuwaelewesha wananchi na kila sekta wajione kwamba wana jukumu la kuitekeleza sera hiyo.

"Suala la Uwezeshaji ni kwa wananchi wote na sio tu wajasiriamali wadogo au watu fulani kila mtu anahusika kwa nafasi yake" alisema Mhe. Waziri.

Vilevile Mhe. Mwambe alisema kuna haja kama nchi kutengeneza mabilionea na wasitokee kama ajali tuu. Hivyo Baraza lina kazi kubwa ya kuwainua na kuwalea watu ambao baadaye wanaweza kuja kujivunia.

Baraza pia linapaswa kuwajengea uwezo wajasiriamali wanaoonekana wana uwezo wa kufanya vizuri na kutoa ajira kwa watu wengine. Hii ni pamoja na kuwapa ushauri na kuwapendekeza kupata mikopo nafuu na sehemu wanazoweza kupata na hata vitendea kazi kama machine za kisasa ili kuongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa wananchi wengine.

Sambamba na hayo Waziri ameitaka menejimenti ya Baraza kupeleka kwenye mafunzo watumishi wake. "Hili mnaweza kufanya kwa kuwatafutia ufadhili kutoka nje, lakini pia hata kozi fupi fupi. Hili litasaidia kuwajengea uwezo watumishi jambo ambalo litakuwa na tija kwa Baraza katika kuwawezesha wananchi" Aliongeza Mhe. Waziri.

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza Bibi Beng'i Issa alimueleza Waziri mipango ya Baraza katika kuhakikisha inafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wananchi.

Baadhi ya mipango hiyo ni kuandaa sera ya Taifa ya ushiriki wa watanzania katika Uwekezaji na miradi ya kimkakati kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kuendeleza vituo vya uwezeshaji katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri, kuratibu utendaji wa jukwaa la wanawake kiuchumi katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri na ujenzi wa jengo la Ofisi kwa ajili ya matumizi ya Baraza.

Kwa niaba ya Bodi ya Baraza Prof. Lucian Msambichaka alimshukuru Mhe. Waziri kwa ujio wake na kwa maelekezo aliyoyatoa na kuahidi kuyafanyia kazi.

"Niseme tuu kwamba Waziri amepata Wizara na Wizara imepata Waziri" alisisitiza Profesa Msambichaka.

Tanzania Census 2022