Habari

Imewekwa: Jul, 03 2020

DHANA YA USHIRIKISHWAJI WA WATANZANIA KATIKA MIRADI ENDELEVU YA KIMKAKATI NA UWEKEZAJI NCHINI (LOCAL CONTENT).

News Images

Mwaka 2004 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilitunga sera na sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Mpaka kufikia mwaka 2016 Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lilizindua mkakati rasmi wa kuhakikisha kwamba Watanzania wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi waTaifa.

Akiwasilisha hoja hiyo Bungeni – Dodoma (5/6/2020), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema;

“Ushiriki wa Wananchi katika uchumi ni suala linalopewa kipaumbele katika Mataifa mengi Ulimwenguni, ukitaka Taifa lako liweze kupiga hatua za kimaendeleo na hasa katika kuhakikisha kwamba uchumi wako unahusisha Jamii na Wananchi kiujumla dhana hii ya local content ni muhimu sana”.

Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Rais. Dkt. John Pombe Magufuli imeweka dhamira ya dhati katika kuhakikisha kwamba, uchumi wa Tanzania ya Viwanda na miradi ya kimkakati inahususha na kujengwa na Watanzania wenyewe.

“Hivyo basi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilitulazimu tujipange na dhana ya ushiriki wa Wananchi (Local content) kama moja ya nyenzo muhimu sana ambayo kwanza, itawasaidia Wananchi katika ujenzi wa uchumi na pili kuliwezesha Taifa kufikia malengo ya uchumi wa kati”. Alisema Mhe. Mhagama.

Kwa namna ya pekee Mhe. Jenista Mhagama alimpongeza Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Beng’i Issa na timu yake juu ya kuonesha jitihada kubwa, katika kusimamia vizuri Sera wezeshi ya Local content.

Aidha Mhe. Waziri Mhagama amewasilisha shukrani zake kwa Kamati ya Katiba na Sheria kwa kutoa miongozo na kutaka kujua ni kwa jinsi gani, Ofisi ya Waziri Mkuu imepiga hatua kwenye dhana hii tajwa ya Local content.

Kwa nafasi yake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bi. Beng’i Issa alikaribishwa kuwasilisha taarifa fupi juu ya utekelezwaji wa Local Content katika miradi endelevu Nchini na jinsi mtazamo huu wa ushirikishwaji wa Wananchi unaosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu umewawezeshaje Watanzania mpaka sasa.

Katibu Mtendaji amewasilisha mambo makuu yapatayo nane katika taarifa hiyo ikiwemo; muundo wa uratibu wa Sera, sekta za kipaumbele, dhana ya tafiti ya Local content, maeneo ya kipaumbele, utekelezaji wa local content, mafanikio, changamoto pamoja na mipango ya baadae.

Katibu Mtendaji amehainisha maeneo muhimu ya kutazamia katika kuratibu ushiriki wa Watanzania katika uchumi kutokana na uwekezaji pamoja na viwanda. Maeneno hayo ni pamoja na ajira na mafunzo, ushiriki wa kampuni za ndani, ujuzi, teknolojia na tafiti, uwekezaji wa kiuchumi kwenye jamii.

“Haya mambo manne ni muhimu sana ambayo yanaleta thamani ya ziada katika uchumi wa Taifa letu” aliongezea Bi. Beng’I Issa.

Vilevile katika utekelezaji wa Local content sekta muhimu zimetajwa kupewa kipaumbele kama sekta kiongozi, sekta hizo ni pamoja na Sekta ya Uziduaji (Madini, Mafuta na Gesi), Sekta ya Ujenzi, Usafirishaji na Mawasiliano, Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Sekta ya Viwanda na Biashara, Sekta ya Utalii pamoja na Sekta mtambuka (Elimu, Ajira, Sayansi na Teknolojia, Ununuzi wa Umma, Fedha na Bima).

Kiujumla utekelezaji wa Local content katika miradi ya kimkakati na uwekezaji umeonesha kuwa na mwenendo mzuri wa mafanikio;

Kwenye eneo la ajira, sekta ya ujenzi na uchukuzi katika mradi wa SGR umeajiri Watanzania wapatao 82% ya wafanyakazi wote, mradi wa Reli umeajiri Watanzania wapatao 91%, mradi wa uwanja wa ndege uliajiri Watanzania wapatao 95%, mradi wa barabara Ubungo umeajiri Watanzania wapatao 95% na mradi wa salenda umeajiri Watanzania wapatao 91% ya wafanyakazi wote katika mradi.

Sekta ya kufua uziduaji wa nishati katika mradi wa kufua umeme umeajili Watazania wapatao 88% ya wafanyakazi wote, mradi wa Maurel et Prom umeajiri 96%, mradi wa Songas umeajiri Watanzania wapatao 96% ya wafanyakazi katika mradi, mradi wa Pan African Energy Tanzania umeajiri Watanzania wapatao 98% na sekta ya madini imeajiri takribani 97% ya wafanyakazi Wakitanzania katika miradi Nchini.

Mafanikio mengine katika Local content, Agenda hii hivi sasa ni mtambuka, imewekwa kwenye Sheria za Madini, Nishati, PPP, Huduma ndogo za Fedha, Bima, Ununuzi huduma za Meli, pamoja na sheria zote zinazitengenezwa hivi sasa, kuteuliwa kwa waratibu wapatao 300 katika Wizara, Idara na Taasisi za Umma, Kutengenezwa kwa tovuti ya Local content, kuzindua muongozo wa Kitaifa wa Local content katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kufanya tafiti bainifu za local content, kufanya uhamasishaji wa ushiriki wa Watanzania katika miradi yote ya kimkakati pamoja nakufanya makongamano ya Local content.

Pamoja na mafanikio hayo, dhana ya Local content ina changamoto ikiwemo ukosefu wa ujuzi, uzoefu na mitaji ya kutekeleza miradi mikubwa, pamoja na ukosefu wa bidhaa na huduma zinazokidhi viwango.

Aidha Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, limeandaa mipango ya baadaye katika utekelezaji wa Local content nchini imiwemo kuandaa mfumo wa kielektroniki na kufuatilia utekelezaji wa Sera hii, kutengeneza kanzidata ya watoa huduma nchini, kutengeneza makakati wa Taifa wa kufuatilia utekeklezaji wa Local content na kuendelea kutoa elimu ya Local content kwa wadau mbalimbali.