UTANGULIZI
Shirika la kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji wananchi kiuchumi imebaini kuwepo kwa mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kutoa ajira nchini. Hata hivyo, pamoja na uwepo wa fursa kubwa inayotolewa na sekta binafsi katika kuziba pengo la uchache wa ajira rasmi nchini sehemu kubwa ya sekta binafsi haijarasimishwa. Kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2020/2021 (Intergrated labour force survey), Sekta isiyo rasmi inashika nafasi ya pili kwa kuajili watu wengi nchini hata hivyo kuto rasimishwa kwake kuna punguza idadi ya watanzania waliopata ajira zenye staha (Decent work). Ajira zenye staha ni fursa ya kufanya kazi ya uzalishaji na inayotoa kipato kinachostahili, uwepo wa usalama mahala pa kazi na hifadhi ya jamii, matarajio ya kujiendeleza n.k. Kwa kuona changamoto hii ya msingi, Shirika la kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na Baraza la uwezeshaji (NEEC) liliweza kuandaa mwongozo wa urasimishaji wa biashara kwa wajasiriamali wadogo na wa kati nchini. Aidha baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi limeendelea kushirikisha wadau wengine wa sekta binafsi kuweza kushirikiana nao kuhakikisha mwongozo huu unatumika kuwafikia wajasiriamali kote nchini kupitia mafunzo ya moja kwa moja yanayotolewa na watoa huduma za maendeleo ya biashara kwa uratibu wa Baraza la Taifa la uwezeshaji kiuchumi.
MALENGO YA JUMLA
Malengo ya mradi huu ni kufikia wafanyabiashara kote nchini kuweza kurasimisha biashara zao na hivyo kupunguza kiwango cha biashara zisizo rasmi ili kuongeza ajira zenye staha nchini.
-
- Kutoa mafunzo kwa wafundishaji ili kupeleka utaalamu na ujuzi wa urasimishaji wa biashara kwa wajasiriamali wadogo na wa kati
- Kutoa mafunzo na uhamasishaji kwa wajasiriamali wakubwa na wadogo kuweza kurasimisha biashara zao.
- Kujenga uelewa wa manunuzi ya umma kwa wafanyabiashara wa kitanzania ili kujenga hamasa ya kurasimisha biashara.
MAFUNZO YA URASIMISHAJI
Katika kipindi cha miezi sita iliyopita Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi limeweza kushirikiana na taasisi mbalimbali binafsi kuweza kuwafikia watanzania wafanyabiashara ili kuweza kuongeza maarifa na utayari wao kuweza kurasimisha biashara zao nchini. Taasisi hizo ni pamoja na shirika la kazi duaniani (ILO), Shirika la maendeleo la MEDA na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Aidha mafunzo hayo yaliweza kufanyika katika mkoa wa Tanga,Mwanza,Geita Lindi,Kagera,Shinyanga,Singida, Dodoma,Kigoma, Simiyu, Tabora,Mtwara na Ruvuma. Mafunzo haya yameweza kufikia jumla ya watanzania 558 (Wawanawake 335 na Wanaume 223) ikijumuisha wajasiriamali na watoa huduma za maendeleo ya biashara.
MIPANGO YA BAADAE
Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi linakusudia kuwafikia watanzania wafanyabiashara kwa maelfu nchi nzima ili kuongeza chachu na utayari wa watanzania wajasiriamali kuweza kurasimisha biashara zao. Mipango hii ya Baraza la uwezeshaji inategemea bajet ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ili kuweza kuratibu jukumu hili la msingi linaloweza kuongeza kiwango cha watanzania waliorasimisha biashara zao na hivyo watanzania kupata ajira zenye staha nchini.