Habari
Dkt. Ashatu awataka wanufaika wa mikopo kurejesha kwa wakati

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ametoa agizo hilo jana (14/05/2022) alipokuwa akihitimisha Maonesho ya Tano ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyofanyika kwa siku saba mfululizo katika Uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.
“Natambua uwepo wa changamoto hii kwa muda mrefu, hususan kwa wanufaika wa mikopo ya 10% (Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu) inayotolewa na Halmashauri zetu. Hivyo naagiza ufuatiliaji wa karibu wa mikopo hii ili tuweze kunufaisha watanzania wengi zaidi kutokana na marejesho hayo” alisema Dkt.Kijaji
Aidha, Dkt. Kijaji ameliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuimarisha uratibu wa mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu na tathimin ya mifuko hii pamoja na programu zake.
Kwa nafasi yale Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Bibi Beng’i Issa alitoa shukrani zake za dhati kwa Mgeni Rasmi kwa kuweza kufika katika hafla hiyo ya kuhitimisha maonesho ya Tano ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji yenye kauli mbiu “Uchumi Imara kwa Maendeleo endelevu” katika kanda hii ya Mashariki.
Katibu Mtendaji alisema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuwezesha Wananchi kiuchumi ikiwemo kuanzisha programu mbalimbali ikiwemo mpango wa kuendeleza viwanda vidogo na vya kati ujulikanao kama SANVN Viwanda Scheme ambayo mpaka sasa umetoa mikopo yenye thamani ya TZS. 1,746,557,651 kwa Miradi 32 iliyo katika Mikoa 8.
“Hii ni moja tu ya jitihada hizo ambazo zinalenga kuimarisha uchumi wa Wananchi, hivyo nitoe shukrani za dhati kwa Serikali na wadau wa kimaendeleo kuweza kulifanikisha jambo hili” alisisitiza katibu Mtendaji
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Uwezeshaji Bibi Anna Maembe alisema jitihada nyingi zinafanywa na Baraza ili kuhakikisha kwamba fursa zipatikanazo katika mifuko na programu za uwezeshaji zinafahamika zaidi kwa wananchi.
“Nitoe ombi kwa Serikali kuendelea kuboresha utendaji kazi wa mifuko ya uwezeshaji na kuongeza mitaji ili mifuko hii iweze kutoa huduma kwa wananchi wengi hususan wa maeneo ya vijijini” aliongezea Mwenyekiti
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuchochea Kilimo Tanzania - TACT ambao ndio wadhamini wakuu wa maonesho haya alisema wanajivunia kudhamini maonesho haya wakiwa kama mfuko wa uwezeshaji kwani lengo ni kuhakikisha mifuko ya uwezeshaji inaleta tija ya maendeleo kwa Taifa kama isemavyo kauli mbiu ya maonesho hayo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigella ametoa shukrani zake kwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji lililo chini ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kuchagua kufanya maonesho haya ya tano ya mifuko na programu za uwezeshaji katika Mkoa wa Morogoro.
Shigella amewataka Wananchi wa Morogoro kuendeleza ushirikiano ulioibuka kipindi hiki cha maonesho na kutumia mahusiano hayo kuendeleza uchumi wao kwani ni bahati kupata fursa kama hiyo ya kiuchumi.
Mwishoni mwa hafla hii Dkt. Kijaji alikabidhi vyeti na tuzo kwa washindi wa maonesho, hati za ruzuku za Milioni 5 zilizotolewa kwa shule mbalimbali na Mfuko wa Misitu Tanzania – TaFF, zana mbili za kilimo (Combine Harvester) pamoja na trekta aina ya NEW HOLLAND TT55 vyotehivi kupitia Kampuni tanzu ya PASS TRUST ijulikanayo kama PASS LEASING COMPANY.
Maonesho haya yanatarajiwa kufanyika tena mwakani katika kanda ya Magharibi hivyo Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) linawakaribisha wadau wengi zaidi kujiandaa ili waweze kushiriki katika maonesho hayo.