Habari

Imewekwa: Jan, 03 2020

TATHIMINI YA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA VIJANA AWAMU YA KWANZA YALIYOFANYIKA MWAKA 2019.

News Images

Mafunzo ya Ujasiriamali kwa Vijana Awamu ya kwanza ya Mwaka 2019 yalifunguliwa rasmi Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista Mhagama mnamo Tarehe 30/7/2019 na yanaratibiwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Lengo la Mafunzo haya ni Kuwahamasisha Vijana Kurasimisha Biashara zao, kuwapa Elimu juu ya Usimamizi wa Biashara zao, kuhakikisha kwamba Vijana wanajitambua kuwa wao ni Wajasiriamali ili kuweza kuendana na Sera ya Nchi ya Uchumi wa Kati wa Tanzania ya Viwanda.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Bi Beng’i Issa ametoa tathimini ya Mafunzo ya awamu ya kwanza kwa Vijana Wajasiriamali Mwishoni mwa Mwaka 2019 yaliyowafikia vijana wa Kitanzania wapatao 1390 katika Mikoa nane ya Tanzania ikiwemo Dodoma, Mwanza, Geita, Lindi, Ruvuma, Tanga, Arusha na Mbeya.

“Mafunzo haya yamewafundisha Vijana Kujitambua kama Wajasiriamali, kuwa na Malengo na vilevile kupiga Hatua katika Biashara zao, pia ushiriki mzuri wa vijana haswa wenye Ulemavu katika mikoa yote nane ambao ni Wajasiriamali ni Jambo la Kujivunia na tungependa wawe kama chachu kwa vijana wengine” Alisema Katibu Mtendaji

Mpango wa Mafunzo ya Ujasiriamali Kwa Vijana wa Mwaka 2019 umelenga vijana 150 katika makao Makuu ya Mikoa nane ya awamu ya Kwanza ya programu.

“Jambo ambalo tumejifunza ni kwamba Vijana wengi wanatamani na wangependa sana kushiriki Mafunzo haya, hivyo itabidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo ili tuweze kuwafikia Vijana wengi zaidi katika Awamu inayofuata” Bi Beng’i M. Issa

Aidha Katibu Mtendaji amesema kwamba Vipaumbele vya Mafunzo haya ni vilevile isipokuwa changamoto zilizojitokeza awamu ya kwanza lazima zifanyiwe Kazi ikiwa kama Hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mafunzo hayo.

Pia Bi Beng’i Issa kaeleza umuhimu wa Kuwahusisha baadhi ya Vijana ambao wamefuzu Mafunzo hayo ya awamu ya Kwanza ili kupata fundisho kutoka kwao na vilevile kuwatumia vyema kama Mashuhuda katika Programu inayofuata katika Mikoa mingine iliyobaki mwaka huu 2020.