Habari

Imewekwa: Feb, 19 2021

HADI SASA KWENYE MIRADI YA KIMKAKATI KUNA MAKAMPUNI ZAIDI YA 1000 YA KITANZANIA YALIYOPEWA ZABUNI NA WAWEKEZAJI

News Images


Hayo yamesemwa leo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi. Beng'i Issa wakati akizungumza kwenye kituo cha redio ya Uhuru FM live kwenye kipindi cha Hello Tanzania Asubuhi hii.

Katibu Mtendaji alieleza kuwa Baraza pia linahakikisha Watanzania wanashiriki katika miradi ya kimkakati. Na hili linafanyika kwa Baraza kutengeneza programu zinazowasaidia Wajasiriamali wa chini na wa kati.

"Hadi tunavyozungumza hivi sasa kwenye miradi ya kimkakati kama SGR, Julius Nyerere Hydropower na mingineyo kuna makampuni ya kitanzania zaidi ya 1000 yaliyopata zabuni au tenda na kufanya kazi na wazabuni wakuu.

Si hilo tuu, Baraza linahakikisha wawekezaji wanahamisha ujuzi kwa watanzania ili pindi mradi unapoisha ujuzi unabaki nchini.

Katibu Mtendaji alisema kuwa Baraza pia lina kazi ya kuwezesha Jamii inayozungukwa na miradi ili ifaidike na miradi hiyo.

Hii inaweza kuwa kwa Mzabuni kujenga kituo cha Afya au Zahanati, ujenzi wa madarasa na kadhalika.

Aliongeza kuwa Baraza pia linasimamia Wananchi waweze kupata mitaji. Katika hilo Baraza linasimamia Mifuko ya Uwezeshaji ambayo kwa namna moja au nyingine inatoa mitaji kwa Watanzania.

Kuna Mifuko ya utoaji huduma, Mifuko inayotoa mikopo bila riba, Kuna Mifuko inayotoa dhamana, Kuna Mifuko inayotoa ruzuku, na Mifuko inayotoa mikopo moja kwa moja kwa Wananchi.

Vile vile kwenye kazi na ajira tunahakikisha Watanzania wanashiriki kwenye miradi kuanzia kwenye ngazi ya utawala hadi ngazi ya vibarua na biashara.

Katika hili Baraza linayataka makampuni ya uwekezaji yahakikishe kuwa yanaajiri Watanzania katika idara ya kiutawala, isipokuwa katika nafasi ambazo hakuna Mtanzania mwenye ujuzi husika. Vibarua pia wawe ni Watanzania na mama ntilie waruhusiwe kufanya biashara zao za chakula bila shida yoyote.

Sambamba na hilo tunataka kuhakikisha kuwa Taifa letu linakuwa na vijana wabunifu kwa kuwa na mitaala bora vyuoni ambayo itawawezesha kuwa wabunifu na hata wakimaliza masomo waweze kuanzisha biashara ambazo wataziendeleza.

Baraza pia linawaangalia wanawake kwa jicho la pili kwani Uchumi wa Nchi hauwezi kuundwa na wanaume tu.

Kuna program ambayo Baraza inashirikiana na Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi ya Umma ili kuwawezesha wanawake kushiriki katika manunuzi ya Umma.

Hata katika miradi ya kimkakati Baraza huwa linahakikisha kwamba linapata taarifa ya idadi ya wanawake walioajiriwa katika miradi hiyo.

Vile vile Baraza linasimamia vikundi vya vikoba 200,000. Katika hili kuna sheria ndogo ya Fedha ya mwaka 2018 iliyoundwa ambayo kwa sasa inasaidia sana vikundi hivi hasa wale waliokuwa wakipoteza Fedha zao.

Kwenye viwanda vyetu vya ndani bado tuna upungufu wa malighafi. Niwaombe Watanzania wazalishe malighafi kwa wingi ili kuvitosheleza viwanda na malighafi zitoke hapa hapa nchini.

Ila Kuna maeneo ambayo kama Taifa tunafanya vizuri kwenye uzalishaji, mfano eneo la ujenzi. Simenti inayotumika kwenye miradi ni hapa hapa, mchanga na kokoto pia ni vya hapa hatuagizi hivyo hatuna budi kuongeza uzalishaji kwenye maeneo mengine pia ili tuweze kujitegemea.

"Niwasisitize Watanzania kurasimisha biashara zao ili waweze kukua kutoka pale walipo na kuinuka Kiuchumi." Aliongeza Katibu Mtendaji.

Tunamshukuru Mhe. Rais Dr. John Pombe Magufuli kwa kuwapatia vitambulisho Wajasiriamali wadogo ambapo lengo la Serikali ni kuona Wajasiriamali hao wanakua na kurasimisha biashara zao ili waweze kuzalisha zaidi na kufanya biashara kubwa ili kutengeneza faida ya kutosha.