Habari

Imewekwa: Mar, 31 2021

​HITIMISHO LA AWAMU YA TATU YA MAFUNZO YA UENDELEZAJI WA BIASHARA MKOA WA GEITA

News Images

HITIMISHO LA AWAMU YA TATU YA MAFUNZO YA UENDELEZAJI WA BIASHARA MKOA WA GEITA

Baraza la Tifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) walianzisha programu ya uendelezaji wa Biashara Mkoani Geita (Geita Enterprise Development Program - GEDP). Programu hii ilizinduliwa na Katibu Mkuu Sera, Uratibu na Uwekezaji Bibi Dorothy Mwaluko Tarehe 20/07/2020, lengo kuu likiwa ni kuwawezesha wajasiriamali wa Mkoa wa Geita kukidhi vigezo na viwango katika kuwania zabuni zitolewazo na Mgodi wa Geita kupitia mafunzo maalumu.

Kupitia program hii Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limekuwa likiratibu mafunzo kwa wajasiriamali hawa ili kuwajengea uwezo katika nyanja mbalimbali za kibiashara na uchumi. Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limeendesha mafunzo haya kwa awamu tatu mpaka kufikia mwezi Machi mwaka 2021 tangu kuanzishwa kwa programu hii.

Kwa kushirikiana na SIDO – Geita, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) liliweza kuratibu awamu ya tatu ya mafunzo kwa vitendo iliyowahusisha Wajasiriamali wapatao 150, awamu hii iliyoanza mnamo Tarehe 8 na kumalizika Tarehe 19 mwezi Machi 2021 kama sehemu ya program hii.

Katika kuhitimisha mafunzo haya kwa niaba ya Katibu Mtendaji; Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi (NEEC) Bw. Julian Mutunzi alisema mradi huu ni kwa ajili ya wajasiriamali wa Mkoa wa Geita na vitongoji vyake, hii ni fursa na nafasi ya upendeleo kwao hivyo hawana budi kuitumia vizuri.

“Tulianza na mafunzo haya na hatua ya mwanzo mwezi Novemba 2020 ambayo tuliyaita mafunzo ya awali na yaligusa mambo ya msingi ya biashara ikiwemo kutunza kumbukumbu na vigezo vya kuwania zabuni katika Mgodi wa Geita, kisha tukafanya mafunzo ya pili ya kongano ili kuwaunganisha wajasiriamali wa Geita na sasa kwa kushirikiana na SIDO – Geita leo tunahitimisha mafunzo ya tatu kwa vitendo” alisema Bw. Julian Mutunzi.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Mgodi wa Geita (GGML) Bw. Reward Tenga amewapongeza wajasiriamali hao kwa maudhurio yao katika kipindi chote cha mafunzo na amewataka waendeleze ujuzi walioupata katika kipindi hicho cha mafunzo katika kukua kibiashara.

Naye Meneja wa SIDO Geita Bw. Japhary Donge amewahasa wajasiriamali waliopata nafasi ya kushiriki katika mafunzo ya vitendo kuelekeza nguvu zao katika kufungua viwanda kama njia ya kumuenzi Hayati Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

“Nawashukuru sana wanafunzi wote kwa vile ambavyo mmekuwa mkishiriki na kuuliza maswali mengi yenye tija na naamini kabisa kwa vitu mlivyovifanya na kujifunza mko mahiri kabisa kuweza kuanzisha biashara katika vikundi hivi, nawakaribisha tena SIDO” aliongezea Bw. Donge.

Aidha, mwakilishi wa wajasiriamali Bi. Scola Charles Njige ametoa shukrani kwa Baraza la Uwezeshaji, Mgodi wa dhahabu wa Geita na SIDO – Geita kwa kufanikisha mafunzo haya na ametoa wito kwa wajasiriamali wengine kutumia fursa kama hizi za mafunzo katika kuendeleza ujuzi ambao utasaidia katika kukuza biashara zao.