Habari

Imewekwa: Jun, 21 2019

Kongamano la Uwezeshaji Kisarawe lazinduliwa

News Images

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Raisi ,Tamisemi Mheshimiwa Suleiman Jafo amezindua Kongamano la Uwezeshaji katika Wilaya ya Kisarawe ambalo limelenga kuandaa mazingira bora kwa wajasiriamali walio kwenye vikundi vya uzalishajimali hapa nchini na jumuiya za kifedha zikiwemo SACCOSS na VICOBA.

Kongamano hilo la siku tatu limeandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambapo taasisi mbalimbali za urasimishaji wa biashara, Mabenki na Mifuko ya Uwezeshaji walipata nafasi ya kutoa mafunzo ya Uwezeshaji kwa wajasiriamali.

Moja kati ya mambo yaliyojadiliwa katika Kongamano hilo ni pamoja na uanzishaji wa kituo cha Pamoja Cha Uwezeshaji katika Wilaya ya Kisarawe ambacho kitakutanisha watoa huduma za kifedha na taasisi za urasimishaji wa biashara na mafunzo ili kumuondolea mzigo mjasiriamali.

Akizungumza kuhusiana na suala hilo Katibu Mtendaji wa Baraza Bibi Beng’i Issa amesema kuwa kituo cha Uwezeshaji cha Kahama kilianzishwa kama mfano lakini lengo hasa ni kuwa na vituo kama hicho kwa nchi nzima ili kuwaondolea usumbufu wajasiriamali wanaotafuta mitaji, elimu, taarifa za masoko na kurasimisha biashara zao.

“Mwaka jana kwa maelekezo ya Waziri Mkuu tulifanikiwa kuanzisha kituo cha Uwezeshaji katika Wilaya ya Kahama hivyo ni vema sasa Wilaya nyingine zote zikaiga mfano huo kwa kujenga vituo vingi zaidi nchini”alisema Katibu Mtendaji.

Kongamano la Uwezeshaji lililofanyika Kisarawe ni moja kati ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye amekuwa akisisitiza umuhimu wa wa Serikali za Mikoa na Wilaya kufanya uhamasishaji wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mikakati mbali mbali ikiwemo makongamano ya wadau wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.