Habari
Maonesho ya tano ya mifuko na program za uwezeshaji na wajasiriamali kuanza tarehe 08/05/2022, Morogoro.

Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng'i Issa wakati wa Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Baraza zilizopo viwanja vya maonesho Nane Nane, Dodoma.
Katibu Mtendaji alisema maonesho hayo ya tano yatahusisha mifuko ya uwezeshaji, Taasisi za fedha, Taasisi za serikali, Taasisi binafsi, Mashirika ya Umma na yasiyo ya umma, mashirika ya kimataifa na wajasiriamali.
"Katika maonesho haya tutakuwa na madarasa mbalimbali yatakayofundishwa kwa wajasiriamali ili kuweza kuwainua kiuchumi na kuwasaidia kurasimisha biashara zao" alieleza Katibu Mtendaji.
Katika Mkutano huo Katibu Mtendaji aliongozana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa kuchochea Kilimo Tanzania (TACT) Dr. John Kyaruzi na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Microfinance Ndg. Mudith Cheyo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TACT alisema kuwa ni heshima kubwa kwao kupata nafasi ya kuwa wadhamini wakuu wa maonesho kwa kuzingatia kuwa wao ni mfuko ambao umelenga kuwainua wakulima wadogo kiuchumi kwa kutumia ardhi zao wenyewe.
"Nawakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro na maeneo ya jirani kutembelea banda letu ili waweze kupata maelezo ya kina zaidi juu ya mfuko wetu na namna unavyofanya kazi" alieleza Dr. Kyaruzi.
Naye Mtendaji Mkuu wa mfuko wa SELF Microfinance alifafanua kuwa lengo la mfuko wao ni kuwakopesha wajasiriamali wa chini, wa kati na wa juu na kuhakikisha wanainuka kiuchumi kwa namna moja ama nyingine.
"Hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu Mfuko wa SELF ulikuwa umetoa kiasi cha Shilingi bilioni 264, Tanzania inakadiriwa kuwa na wajasiriamali milioni tatu (3) ambapo asilimia 75 wamejiajiri wenyewe na hawana shughuli nyingine zaidi ya ujasiriamali" alifafanua Mtendaji Mkuu wa SELF.
Maonesho ya mwaka huu yataanza Jumapili ya tarehe 8/5/2022 na yatazinduliwa tarehe 9/5/2022 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martin Shigella na yatafungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mnamo Tarehe 14/5/2022, Wananchi wote mnakaribishwa kwani maonesho haya ni bure (hakuna kiingilio).
Wadhamini wakuu wa maonesho haya ni Mfuko wa kuchochea maendeleo ya kilimo Tanzania (TACT).