Habari

Imewekwa: Jun, 26 2019

Mikoa na Halmashauri kuanzisha vituo vya Uwezeshaji

News Images

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Bibi Beng’i Issa amezitaka Ofisi za Mikoa na Halmashauri kuzingatia maagizo ya Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) ambayo aliyatoa wakati akifungua Kongamano la Nne la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofanyika Juni 15 mwaka huu katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma.

Moja kati ya maazimio makubwa ambayo alikumbushia ni pamoja na kuzitaka Ofisi za Mikoa na Halmashauri kuanzisha vituo vya uwezeshaji kama kile kilichojengwa Kahama ambacho kimekutanisha taasisi za fedha,masoko,mafunzo na urasimishaji wa biashara.

“Tunazikumbusha Mamlaka za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha zinatekeleza maagizo ya Waziri Mkuu ambayo aliyatoa katika Kongamano la nne la uwezeshaji ambapo alizitaka kuanzisha vituo vya uwezeshaji kwa kuiga mfano wa Halmashsuri ya Mji wa Kahama”alisema Katibu Mtendaji.

Mbali na hili la kituo maagizo mengine ambayo yalitolewa na Waziri Mkuu na kutajwa na Katibu Mtendaji ni kama ifuatavyo.

  1. Mamlaka husika za Serikali zihakikishe zinashirikiana na Sekta binafsi, Wadau wa Maendelo, Asasi za Kiraia na jamii kwa ujumla ili Sera, Mipango na Shughuli zao za kila siku zitoe kipaumbele katika uwezeshaji wananchi kiuchumi.
  2. Wadau wa uwezeshaji kuwasilisha taarifa za uwezeshaji Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji ili ziweze kusaidia katika kuweka mipango mikubwa iliyopo ndani ya Serikali.
  3. Mikoa ya Dar Es salaam, Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa, Singida na Shinyanga ihakikishe kuwa inaandaa Investment Guide kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao;
  4. Mikoa iliyokamilisha investment Guide kuhakikisha inatumia fursa zilizoainishwa pamoja na kuweka mikakati ya utekelezaji ikiwemo kutangaza fursa zilizoko katika kila mkoa;
  5. Kuhakikisha kuwa fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi zilizobainishwa kupitia tafiti zilizowezeshwa na kufadhiliwa na UNDP zinafanyiwa kazi kwa kuhakikisha kuwa Miradi mikubwa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inatokana na tafiti hizo;
  6. Kuratibu masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2015-2020 kuhusu uanzishwaji waViwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu; na
  7. Mifuko ya Uwezeshaji kuongeza ufanisi ili iweze kuwafikia watanzania wengi. Mfumo wa kupima Mifuko ya Uwezeshaji kwa Matokeo yao kiuchumi na kijamii na siyo kwa shughuli walizofanya ukamilike na Ofisi yangu iuzindue kwa utekelezaji.