Habari

Imewekwa: Jun, 23 2021

​MRADI WA SANVN VIWANDA SCHEME ULIVYOZAA MATUNDA KWA WAJASIRIAMALI NCHINI

News Images

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng’i Issa akiambatana na wawakilishi wa Shirika la Kuendeleza Viwanda vidogo Tanzania SIDO, wametembelea kiwanda cha Woodmont Napkins kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za tishu kilichopo eneo la viwanda vidogo yaani SIDO Industrial Estate Area Jijini Dar es Salaam.

Woodmont Napkins ni kiwanda pekee kinachozalisha tishu kinachomilikiwa na Mtanzania ambaye ni mmoja wa wanufaika wa programu ya SANVN VIWANDA SCHEME inayoratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Taasisi ya SIDO, Benki ya Azania, NSSF na VETA.

Katika ziara hiyo Katibu Mtendaji alisema moja ya malengo ya programu ya SANVN VIWANDA SCHEME ni kuhakikisha baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda kutoka nje ya Nchi zinazalishwa na Watanzania wenyewe kwani bidhaa nyingi za muhimu hazizalishwi na viwanda ndani.

“Tunajivunia kuona mmoja kati ya wanufaika wa mwanzo kabisa wa programu yetu ya SANVN VIWANDA SCHEME amepiga hatua katika uzalishaji wa bidhaa hii ambayo inaendelea kukua kwa kasi, tumekuja kuona maendeleo yake na jinsi ya kutatua changamoto mbalimbali za kibiashara ambazo anakutana nazo” aliongeza Beng’i Issa

Vilevile Katibu Mtendaji alisema kutokana na uhitaji wa bidhaa hiyo kuwa mkubwa hasa katika miradi ya kimkakati ambayo inakusanya watu wengi sehemu moja, kuna haja ya kuangalia ni jinsi gani kiwanda hicho kitasaidiwa ili kiweze kuzalisha zaidi na pengine kuongeza bidhaa nyingine zitakazokidhi mahitaji.

Kwa nafasi yake Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Nathan Tibaigana amesema SANVN VIWANDA SCHEME imemuwezesha kukuza biashara yake na kupiga hatua katika uzalishaji wa bora zenye ushindani katika soko.

Aidha, Bw. Nathan ametoa shukrani zake kwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji kwa kumtembelea na kuangalia maendeleo yake kiwandani hapo na kuwashauri vijana wasiogope kujitosa katika fursa za ujasiriamali kwani Serikali ipo ili kuwaunga mkono katika uendekezaji wa Biashara zao.