Habari

Imewekwa: Jun, 10 2019

NEEC inajivunia mafanikio lukuki kuwezesha wananchi kiuchumi

News Images

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) linajivunia mafanikio lukuki iliyoyafikia hadi sasa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004 chini ya sheria ya Bunge namba 16 ibara ya (4) ya Sheria ya Uwekezaji, hususani kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19.

Madhumuni ya kuanzishwa baraza hili ni kusaidi kutoa mwongozo kwa watanzania walio wengi kupata fursa za kumiliki uchumi na hata kutoa upendeleo zaidi kwa wananchi katika kunufaika na fursa za kiuchumi zilizopo nchini.

Katibu Mtendaji wa baraza hilo Beng’i Issa ameeleza ofisini kwake wakati baraza likijiandaa kufanya kongamano la nne la NEEC jijini Dodoma baadae mwezi huu.

“Ndugu muandishi, Baraza linajivunia mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake hapa nchini ambapo wananchi hususani wajasiriamali wadogo na wakati wamejenga uelewa mkubwa kuhusu shughuli za baraza na kwa kupitia ofisi za wakuu wa mikoa, jukumu la kuwasaidia limekuwa jepesi zaidi” ameeleza Katibu Mtendaji huyo.

MAFANIKIO YA BARAZA.

Ameyataja baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa ni pamoja na mwitikio mzuri na ushirikiano toka kwa wakuu wote wa mikao ishirini na sita (26) hapa nchini ambapo wamekuwa mstari wa mbele sana kusaidia shughuli za baraza.

Amefafanua zaidi Katibu Mtendaji kwamba, katika kongamano la tatu la NEEC lililofanyika jijini Dodoma mwaka jana June 2018 ambapo Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi, alitoa maagizo kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha mikoa yote inatenga maeneo maalum ya wajasiriamali kufanya shughuli zao ikiwemo ujenzi wa viwanda vidogo,ambapo kulingana na Katibu Mtendaji huyo, agizo hili limetekezwa kwa asilimia mia moja, amesema Bi Issa.

“Ninawashukuru sana wakuu wote wa mikoa hapa nchini kwa jinsi walivyotekeleza agizo la Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa kuhakikisha mikoa inasimamia wilaya na halmashauri husika kutenga maeneo ya wajasiriamali wadogo ili yawe ya kufanya biashara pamoja na ujenzi wa viwanda vidogo, agizo hili wamelitekeza vizuri sana”

FEDHA ZA MAKUNDI MAALUM.

Pia amefafanua Katibu Mtendaji kwamba, katika suala la kutenga asiliami 10 kila halmashauri au wilaya kwa ajili ya makundi maalum mpango huu umetekelezwa vizuri sana. Ametaja fedha za akina mama 4%, vijana 4% na walemavu 2% zimetengwa kwa usimamizi mzuri wa wakuu wa mikoa nchini. Pia amesema, “hadi sasa zaidi ya 50% ya mawasilisho ya fedha zilizotarajiwa kutengwa zimeshawasilishwa na taarifa husika imeshafikishwa kwenye baraza toka ngazi za ofizi za wakuu wa mikoa” amefafanua Katibu Mtendaji.

VITAMBULISHO VYA WAJASIRIAMALI WADOGO.

Mafanikio mengine aliyoyabainisha Katibu Mtendaji wa NEEC ni mwitikio mzuri na mkubwa wa zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo vilivyotolewa na ofisi ya Rais kwenda kwa wakuu wa mikao nchini ili vigawanywe.

“Tunampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Joesph Magufuli kwa ubunifu huu mkubwa wa vitambulisho vya wajasiriamali, kwani umeongeza imani zaidi kwa kundi hili lililokuwa likiangaika kupata maeneo ya kufanyia biashara ili kujikwamua kiuchumi” amefafanua Bi Issa.

Amesema pia kwamba hadi mwishoni mwa mwezi Mei 2019, takribani ofisi za wakuu wote wa mikoa hapa nchini walishawasilisha taarifa zao kuhusu zoezi hili kwa baraza (NEEC) na kuonesha jinsi zoezi la ugawaji vitambulisho hivyo lilivyofanikiwa. Ametaja kiasi cha fedha zilizokusanywa hadi wakati huo kuwa ni zaidi ya shilingi bilioni ishirini zimeshakusanywa na serikali. Pia ameongeza kwamba “baraza linatarajia kuona mafanikio chanya zaidi kwa mwaka ujao wa fedha kutoka kwenye kada hii ya wajasiriamali wadog”amefafanua zaidi Katibu Mtendaji.

KITUO CHA UWEZESHAJI WANANCHI MJINI KAHAMA.

Mafanikio mengine kulingana na Katibu Mtendaji wa NEEC ni kufanikisha kuanzishwa kwa kituo au ofisi ndogo ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi katika mji wa Kahama uliopo mkoani Simiyu.

Kulingana na maelezo yake Bi Issa amesema kituo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi hususani kwa ukanda mzima wa mikoa ya kanda ya Ziwa ambapo huduma zote zinazotolewa na baraza zinapatikana mjini Kahama na kurahisisha zaidi masuala ya uwezeshaji kwa ujumla. Ameushukuru uongozi wa mkoa wa Simiyu kwa jinsi ulivyosaidia kufanikisha jambo hili.

Ametaja baadhi huduma zilizorahisishwa zikiwepo huduma za usajili biashara (BRELLA), huduma za usajili na ulipaji kodi nchini (TRA), huduma za viwango (TBS), huduma za viwanda vidogo nchini (SIDO) pamoja na zile za mamlaka ya udhibiti wa chakula na dawa (TFDA).

MATARAJIO YA BARAZA KATIKA MWAKA UJAO WA FEDHA.

Baraza la uwezeshaji wanachi kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia masuala ya vijana, ajira na walemavu imepanga kuandaa mafunzo ya pamoja kwa vijana ili kutoa elimu ya ujasiriamali kukuza uelewa ili waweze kufanya shughuli zao kwa mafanikio zaidi.

Pia amefafanua Katibu Mtendaji kwamba, vijana ambao hawajabahatika kupata elimu ya kutosha kwenye sekta maalum za umma, ambao wapo mitaani na vijijini wakifanya shughuli za ujasiriamali watapatiwa mafunzo maalum mwezi huu wa June 2019. Pia vijana walemavu wajasiriamali watapatiwa mafunzo kama hayo mwezi Julai, amefafanua zaidi.

RAI YA BARAZA KWA WAKUU WA MIKOA NCHINI.

Baraza la Uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC) linatoa rai kwa ofisi zote za wakuu wa mikoa nchini kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika mikoa yao ili kurahisisha shughuli za kusaidia huduma kwa wananchi katika maeneo yao.

Akirejea katka kubainisha mafanikio yaliyokwisha kupatikana toka mkoani Simiyu katika mji Kahama ni kwamba, kasi ya kuhudumia wanachi inaongezeka zaidi endapo kila mkoa itaweza kufanikisha kufungua kituo cha huduma ya pamoja, ili shughuli za urasimishaji biashara za wajasiriamali, pamoja na utoaji elimu ya kodi, kujengewa uwezo kupitia mamala ya viwanda vidogo nchini yaani ( SID), udhibiti ubora (TBS), pamoja na huduma za bima za fedha na mikopo zitarahisishwa zaidi.

Baraza linatarajia kufanya kongamono la nne mnamo June 15, 2019 jijini Dodoma ambapo Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na atakabidhiwa orodha ya majina ya maeneo ngazi za mikoa, wilaya na halshauri zilizofanya vizuri zaidi katika kuwezesha shughuli za wajasiriamali ili serikali iwatambue na kuwatunuku tuzo maalum.