Habari

Imewekwa: May, 05 2021

NEEC YATEMBELEA KIWANDA KIDOGO CHA COSIRA KINACHOJISHUGHULISHA NA UZALISHAJI WA SABUNI

News Images

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi likiongozwa na Katibu Mtendaji Bibi Beng’i Issa limefanya ziara mapema leo likiambatana na Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji kutoka SIDO Bibi Shoma Kibende katika eneo la kiwanda hicho kilichopo Kimara Baruti, Wilaya ya Ubungo – Dar es Salaam.

COSIRA ni Kiwanda kidogo kinachomilikiwa na familia moja kilichoanza shughuli zake mwaka 2016 baada ya kurasimisha biashara hii kupitia Taasisi mbalimbali za Serikali ambazo ni SIDO, BRELA, TRA, TBS, TFDA, GCLA na GSI. Hapo awali kiwanda hiki kilikuwa na uwezo wa kuzalisha katoni 50 zenye miche 500 mpaka sasa kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha katoni 100 mpaka 200 zenye miche 1000 mpaka 2000.

Akizungumza katika ziara hiyo Katibu Mtendaji wa NEEC alisema Baraza la Uwezeshaji limekuwa likifanya ziara mbalimbali za kuwatembelea Wajasiriamali katika maeneo tofauti ili kuweza kuwasikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Sambamba na hilo Katibu Mtendaji amesema lengo kuu ni kuhakikisha kuwa Wajasiriamali hawa wanatoka katika hatua moja kwenda hatua nyingine katika nyanja tofauti ikiwemo ubora na viwango katika uzalishaji.

“Dhumuni la Serikali ni kuhakikisha bidhaa kama hizi za sabuni zinatoka ndani ya Nchi kwani uwezo wa kuzalisha na kutengeneza sabuni hizi tunao kitu kikubwa ni kutanua wigo wa uzalishaji na kuhimiza Wananchi kutumia bidhaa hizi za ndani ya Nchi" aliongezea Katibu Mtendaji

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa COSIRA Bibi Adegunda Komba ameiomba Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuwawezesha kupata mkopo ambao utainua uzalishaji na kuongeza ubora wa bidhaa hizo.

“Tunashukuru sana kupata ugeni huu kutoka NEEC, changamoto tunazo nyingi katika nyanja mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa mashine za kisasa, uzalishaji na masoko na kama kampuni tunaamini kwamba Serikali yetu itatutafutia ufumbuzi" alisema Adegunda

Naye Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji kutoka SIDO Bibi Shoma Kibende amesema Kiwanda hiki ni moja ya jitihada za Serikali kupitia SIDO na lengo ni kuhakikisha viwanda vidogo vinapiga hatua.

"Changamoto tumezisikia na nyingine zinaangukia katika upande wetu hivyo tutaangalia ni namna gani ya kupata ufumbuzi kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji" alisema Bibi Shoma Kibende

Aidha, Katibu Mtendaji wa NEEC amewasisitiza Wajasiriamali kwenda na wakati ikiwemo kutumia mitandao ya kijamii katika kutafuta masoko ya bidhaa zao.