Habari

Imewekwa: Sep, 10 2019

Ofisi ya Waziri Mkuu na mkakati wa kupunguza tatizo la ajira

News Images


TAKWIMU za Sensa ya watu na makazi ambayo ilifanyika nchini mwaka 2012 ilionesha Tanzania kulikuwa na watu wasiopungua milioni 50 katika Mikoa yote ya Bara na Visiwani.

Katika idadi hiyo utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014 ulionesha kuwa kundi la Vijana linafanya asilimia56 ya nguvukazi ya Taifa. Wastani huu unawagusa wale walio kwenye rika la kuanzia miaka 15 hadi 35 kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007.

Hii ina maana kuwa nguvukazi ya Taifa hili kwa kiasi kikubwa inategemea uwepo wa kundi la vijana katika shughuli zote za uzalishajimali na kuchochea maendeleo ya nchi.Uwekezaji wowote ambao unafanyika nchini hivi sasa kupitia miradi mbalimbali hauwezi kuliepuka kundi hili.

Kutokana na hali hiyo,Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Kazi, Vijana,Ajira na wenye Ulemavu imekuwa ikiangazia zaidi vijana kupitia program zake za mafunzo kwasababu ndio ambao wameshikilia hatima ya Taifa kwa kila kitu.

Miongoni mwa Programu za ukuzaji ujuzi kwa vijana ambazo zinatekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ni pamoja na mafunzo ya kilimo kwa teknolojia ya kitalu nyumba ambayo inatoa nafasi kwa vijana 100 kwa kila kimoja,mafunzo ya ujasiriamali,mafunzo ya vitendo kazini, urasimishaji wa ujuzi uliyopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na uanagenzi.

Mafunzo haya ya ukuzaji ujuzi yanafanyika kwa kushirikiana na wadau na taasisi za elimu na mafunzo ya ufundi kama VETA, DIT, Donbosco, taasisi za Umma na makampuni binafsi.

Uwekezaji huu wa Serikali kwa kundi la vijana unalenga kuwapa maarifa na mbinu za kuboresha na kukuza biashara zao ili wawe na mchango chanya kwa pato la Taifa.

Ili kuhakikisha idadi kubwa zaidi ya vijana inanufaika na fursa hizi, hivi karibuni Waziri wa NchiOfisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mheshiwa Jenista Mhagama alizindua program nyingine ya mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara ambayo yamepangwa kuwafikia vijana wasiopungua1,200 katika Mikoa nane (8) ya Tanzania Bara.

Shabaha ya mafunzo haya ambayo yanagharamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ni kusaidia vijana kujitambua kama wajasiriamali, kurasimisha biashara zao,uandaaji wa maandiko ya mradi,uundaji wa makampuni ili kupanua wigo wa ajira,kuwaunganisha na fursa za mikopo na ruzuku kutoka kwenye Mifuko ya Uwezeshaji ya Serikali na taasisi za fedha.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa ushirikiano wa Ofisi ya Waziri Mkuu sehemu ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Aidha wadau wengine muhimu katika usimamizi na uendelezaji biashara ambao wanashiriki kutoa mada ni pamoja na SIDO, TBS, TRA, OSHA, TFS, PASS TRUST, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake(WDF), Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF) na taasisi za kifedha zikiwemo Benki za CRDB,NMB, NBC na SELF Microfinance.

Kwa hatua za awali mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara yameshafanyika katika Mikoa ya Dodoma,Ruvuma na Geita.Mafunzo haya yataendelea katika Mikoa ya Mwanza, Lindi, Arusha, Tanga na Mbeya.

Akizungumza Mkoani Geita baada ya kuwakabidhi vyeti wahitimu,Waziri wa Nchi Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha vijana kufahamu dhana nzima ya ujasiriamali, urasimishaji wa biashara, hali ya masoko, fursa zamitaji na mikakati ya uendeshaji wa biashara.

Aliongeza kuwa Ujasirimali ni moja kati ya nguzo za Sera ya Taifa ya Uwezeshaji ambayo inalenga kuinua viwango vya ujuzi na uzoefu wa masuala ya biashara hapa nchini.

“Ofisi ya Waziri Mkuu ipo tayari kuendelea kuwajengea uwezo vijana katika maeneo yote ya nchi na hili litafanikiwa kwa kushirikiana na wadau wa uwezeshaji kutatua changamoto zinazowakabili ili muweze kujiajiri na kuajiri vijana wenzenu,” alisema Mhagama alipokuwa Geita.

Mama Mhagama aliwataka vijana kutumia fursa hiyo kama chachu ya mageuzi katika kuboresha biashara zao.

Nae Mwakilishi wa vijana katika Mkoa wa Geita Bw. Salim Hassan alitoa shukrani zake kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Baraza la Uwezeshaji kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yanaweza kuwa mwanzo mpya katika shughuli zao za uzalishajimali.

“Tunashukuru kwa kupata fursa hii kwani hapo kabla tulihudhuria mafunzo mengi lakini haya ya leo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu yapo tofauti kwani tumeletewa wadau husika kutoka kwenye taasisi za kifedha na Mifuko ya uwezeshaji ambao wametupa maarifa na namna ya kurasimisha biashara zetu na kuziendea fursa za mikopo”alisema kijanahuyo.

Ifahamike kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuipeleka nchi kuwa na uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.Hivyo hiki kinachofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwekeza kwa vijana inaweza kuwa chachu ya kufikia dira na maono ya Serikali.