Habari

Imewekwa: Apr, 13 2021

“SEKTA YA VICOBA IINAFUNDISHA UMUHIMU WA FEDHA, UMUHIMU WA KUWEKA AKIBA NA UMUHIMU WA KUWEKEZA”

News Images

Ameyasema hayo Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng’i Issa katika hafla fupi ya kusherehekea miaka 4 ya YEMCO WALIMU VICOBA iliyofanyika katika fukwe za bahari ya hindi mwishoni mwa juma lililopita.

Katibu mtendaji amesema kundi la walimu ni kundi muhimu sana na amewaomba walimu hao wawe chachu katika jamii kwani elimu ya fedha inahitajika kwa kiasi kikubwa, hivyo ni vyema elimu hiyo itolewe kuanzia ngazi ya chini kabisa ya familia.

“Nina imani kwamba mna uwezo mkubwa sana wa kuisaidia jamii yetu hasa katika hii sekta ya huduma ndogo za fedha kwa sababu kabla hatujafikiria kujiendeleza kuwa wakubwa ni lazima tuanzie kwenye ngazi ya jamii na ndipo VICOBA vilipo” aliongezea Bibi Beng’i

Pamoja na mambo mengine Katibu Mtendaji amewasihi wana VICOBA kuhamasisha watu wengi zaidi hasa wanaume kujiunga katika vikundi hivi kwani takwimu zinaonesha wanavikundi wengi ni wanawake na hasa ukizingatia kwamba huduma hii ni ya watu wote wenye malengo ya kukua kiuchumi.

Kwa mujibu wa Sheria ya huduma ndogo ya fedha ya mwaka 2018 inawataka wana VICOBA kujisajili upya kupitia Halmashauri zao ifikapo Tarehe 30 Mwezi wa 4 Mwaka 2021, Beng’i Issa amewataka wanavikundi kujielimisha juu ya Sheria hii na amewasisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuunda mfumo mzuri wa uendeshaji wa vikundi vya kifedha vya kijamii.

Aidha, Beng’i Issa amewataka wanavikundi kuchangamkia fursa zipatikanazo Serikalini ikiwemo fursa ya SANVN VIWANDA SCHEME iliyoanzishwa na Taasisi tano zikiwemo SIDO, AZANIA, NEEC, VETA na NSSF akiongezea kuwa mpango huu unatoa mikopo nafuu sana kwa Wajasiriamali wenye ndoto ya kuanzisha viwanda vinavyochakata mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Kwa nafasi yake Kiongozi wa VICOBA Tanzania Bw. Bassanga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa YEMCO VICOBA ametoa shukrani zake kwa Katibu Mtendaji wa NEEC kwa kuweza kufika katika hafla hiyo maalum na kuwapatia chakula cha ubongo kupitia nasaha zake.