Habari

Imewekwa: Nov, 27 2019

Elimu kuhusu mfumo wa soko jamii yatolewa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati jijini Dar es Salaam.

News Images

Mfumo wa soko jamii unahakikisha kuwa binadamu ndiye mlengwa mkuu wa shughuli zote za uchumi na kwamba udhibiti wa serikali wa moja kwa moja katika kuendesha uchumi unapunguzwa au kuondolewa kabisa, lengo ni kutoa fursa sawa kwa kila mtu.

“Kwa namna ya pekee ningependa kutanguliza shukrani zangu za dhati kwa Konrad Adenauer Stiftung (KAS), kwa juhudi za maandalizi wa mfumo huu kwa kuanzia utafiti mpaka hatua ya mwisho ya kukamilisha kitabu kinachoelezea mfumo wa uchumi wa soko jamii kwa Tanzania kwa kuelekea maendeleo ya uchumi jumuishi na endelevu”. Alisema Katibu Mtendaji.

Imeelezwa kwamba mfumo huu umebuniwa mahususi kwa ajili ya Tanzania ili kuongeza ukuaji wa uchumi shirikishi na endelevu na kuhakikisha ustawi wa baadae wa nchi yetu. Mfumo huu unaendeshwa kwa nguzo na kanuni hizi; Mshikamano, Uwezo wa kujitengemea na kujiendesha, Ustawi kwa wote, Masoko huru na ushindani wenye tija na Mfumo wa udhibiti wa kisheria.

“Katika mfumo huu wa soko la kijamii, mgawanyo wa rasilimali kama vile bidhaa na huduma, rasilimali watu, mtaji wa ardhi vyote kimsingi vinaratibiwa na soko, shughuli zote za kiuchumi zinaongozwa na soko, mfumo wa ushindani sokoni unategemea bei huria na unalenga kuongeza upatikanaji wa bidhaa adimu na hivyo kuongeza ufanisi katika maendeleo”. Alisema Bibi Beng’i Issa.

Pamoja na mambo mengine yaliyowekwa wazi katika mfumo huo ni kwamba ili shughuli za kiuchumi ziweze kuwa na ufanisi endelevu ni lazima ziwe na mfumo wa kisheria, unaoweka utaratibu kwa kuwa na uchumi imara na serikali rafiki inayozingatia utawala bora.

Wito wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni kuwaomba wadau wote kila mmoja kwa nafasi yake kushiriki katika jitihada za kutekeleza Mfumo huu kwa ujumla na kila Taasisi katika eneo lake kwa lengo la kuwawezesha kuongeza ushiriki wa wananchi katika kumiliki sehemu kubwa ya uchumi wao kupitia shughuli mbalimbali za Uchumi. `