Habari

Imewekwa: Jul, 17 2020

UZINDUZI WA MPANGO WA UENDEKEZAJI WA VIWANDA VIDOGO NA VYA KATI.

News Images

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amezindua Mpango wa Uendelezaji wa Viwanda Vidogona vya Kati wenye lengo la kutatua changamoto ya upatikanaji ujuzi, masoko na mitaji katika miradi midogo nay a kati (SMEs).

Uzinduzi huo uliofanyika Jijini Dodoma Tarehe 10/07/2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Hazina, na kuhudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Profesa Riziki Shemdoe.

Pia Mpango huu unaosimamiwa na Taasisi tano zikiwemo SIDO, Benki ya Azania, NEEC, VETA na NSSF uliudhuriwa na Wakuu wa Taasisi shirika, Viongozi wa Kiserikali na Sekta Binafsi, Wajasiriamali na Wanafunzi kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu Nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mhagama amesema Mpango huu upo kwa ajili ya Wajasiriamali na unalenga kutatua changamoto ya mitaji na ukosefu wa ujuzi katika uzalishaji wa bidhaa Nchini. Hivyo amewataka Wajasiriamali wanaokidhi vigezo kujitokeza kwa wingi ili waweze kupata kuwezeshwa na kuboresha biashara zao.

Aidha Mhe. Mhagama amezitaka taasisi shirika zinazohusika na mpango huu unaoratibiwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, kusimamia nafasi zao katika utekelezaji wa Mpango kwa ufanisi wa hali ya juu.

Pia amesisitiza kuwa mikopo hii itolewe kwa wajasiriamali watakaokidhi vigezo tu bila kuwa na ubaguzi na kuwataka wasimamizi kuwa waaminifu katika mchakato mzima wa utekelezaji wa mpango huu mahususi, unaolenga kuwawezesha Kiuchumi Wajasiriamali wa Tanzania.

Waziri Mhagama ameagiza kutengenezwa kwa kanzidata itakayo onyesha taarifa mbalimbaliza Wajasiriamali watakaopata mikopo ili iwe rahisi kuratibu mwenendo wao na kuona ni jinsi gani ya kutatua changamoto zitakazo ambatana na mpango huu.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako, amesema mpango huu umekuja wakati muafaka kwa sababu utachagiza ukuaji wa Uchumi na kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo Nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa alieleza furaha yake ya uwepo wa mpango huu kwani unagusa sekta muhimu ya viwanda na biashara ambayo inaoanisha sekta ya kilimo, uvuvi na Ufugaji ambazo zina mchango mkubwa katika kukuzauchumi wa Taifa letu la Tanzania.

“Lengo la Mpango huu ni kuhakikisha upatikanaji wa kipato cha kati endelevu kinachogusa Kaya nyingi za Kitanzania, kwani utatengeneza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta mbalimbali za kibiashara” Alisema Waziri Bashungwa.

Kwa nafasi yake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) alisema, mpango umeainisha namna bora ya kuwawezesha Wananchi Kiuchumi ikiwemo kuwapatia mitaji yenye masharti nafuu, kuwapatia mafunzo na kuwasimamia katika shughuli zao za Kijasiriamali.