Habari

Imewekwa: Sep, 12 2022

Uzinduzi wa mwongozo wa kitaifa wa uanzishaji na uendelezaji majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi

News Images

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limeshiriki kikamilifu katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo wa kitaifa wa uanzishaji na uendelezaji majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi nchini.

Hafla hiyo imefanyika siku ya Jumapili, Tarehe 11/09/2022 katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani.

Uzinduzi huo umefanywa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Tukio hilo maalum limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, wanawake wajasiriamali, watumishi wa serikali pamoja na wadau mbalimbali wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Katika hafla hiyo Dkt. Gwajima ametoa agizo kwa wadau wa uwezeshaji kusisitiza wanawake kujiunga na majukwaa wa uwezeshaji wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya hadi Taifa ili waweze kupata sehemu ya kujadili mambo yao kuhusu ujasiriamali na biashara kiujumla pamoja na mambo mengine ya kijamii.

“Hili tutalifuatilia kwa ukaribu ikiwa ni ajenda ya kitaifa na ni ajenda ya watanzania, kama kuna changamoto ya uanzishaji wa majukwaa haya tujadili ili tupate njia sahihi ya kuzitatua” alisisitiza Dkt. Gwajima

Kwa nafasi yake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wanachi Kiuchumi (NEEC) Bibi Beng’i Issa amesema mpaka kufikia Juni 2022 jumla ya majukwaa 26 yameanzishwa katika ngazi ya Mikoa sawa na 100% ya Mikoa yote, katika ngazi ya Halmashauri majukwaa 151 yameanzishwa ambayo ni sawa na 82% ya Halmashauri zote, katika ngazi ya Kata majukwaa 1354 yameanzishwa sawa na 37% ya Kata na katika ngazi ya Vijiji na Mitaa majukwaa 1859 yameanzishwa ambayo ni sawa na 12% ya Vijiji na Mitaa hapa nchini.

“Baraza linatoa shukrani za dhati kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuandaa mwongozo huo ambao utahakikisha usimamizi mzuri na ufuatiliaji wa majukwaa haya, Baraza litaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha majukwaa haya yanaongezeka na kuimarika zaidi” aliongeza Katibu Mtendaji.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amewataka wadau wa maendeleo na uwezeshaji kuja pamoja na kushirikiana ili kufanikisha adhima ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye muasisi wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi.