Habari

Imewekwa: Apr, 22 2021

WAFANYABIASHARA NA WAJASIRIAMALI WA GEITA WATAKIWA KUWA NA DESTURI YA KUWEKA AKIBA PINDI WAFANYAPO BIASHARA ZAO.

News Images

Hayo yalikuwa maneno ya mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndg. Dennis Bandisa wakati akifungua mafunzo ya Wajasiriamali wa Mkoa wa Geita awamu ya nne ambayo yanahusisha uanzishaji wa Kongano (Clusters).

Mafunzo hayo yamekuja baada ya Wakufunzi kupata semina ili pia kuwawezesha Wajasiriamali hao kuelewa maana na umuhimu wa Kongano katika kuendeleza Biashara zao.

Sambamba na kuwaeleza umuhimu wa kuweka akiba Katibu Tawala alieleza kuwa Serikali yetu inabuni mikakati mbali mbali, lengo ikiwa ni kuwakwamua Wananchi kutoka kwenye umaskini.

Si hilo tuu lakini pia mikakati hii inatengeneza ajira. Kwa sababu Wafanyabiashara wanaopata mafunzo lazima wataajiri Watanzania wenzao.

"Niwapongeze Baraza kwa kuweza kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa kuja na mafunzo haya ya Kongano kwa ubunifu mkubwa." Alisema Katibu Tawala.

Alifafanua kuwa Kongano hizi zitawasaidia Wafanyabiashara wa Geita kuweza kushindana katika Zabuni zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita. Lakini ni lazima tuhakikishe Kongano hizi zina uongozi mzuri ili ziweze kuendelea mbele.

"Tusijikite kujengeana uwezo ili tuu tuweze kushinda Zabuni za Mgodini. Tufikirie na maeneo mengine ambayo yatatusaidia kukuza mitaji." Aliongeza Katibu Tawala.

Aliongeza kuwa Mkoa wa Geita umezungukwa na ziwa Victoria ambalo lina tani nyingi za samaki ambapo wafanyabiashara wanaweza kuwekeza huko na kupata mitaji ya kutosha.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng'i Issa aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Geita kwa Ushirikiano mzuri wanaoutoa tangu kuanza kwa mradi huo.

Aliongeza kuwa washiriki watapata fursa nzuri ya kuelewa juu ya uanzishwaji na usimamizi wa Kongano. Vilevile Baraza limeona kuna tija katika utekelezaji wa program hii ya mafunzo hadi kufikia awamu ya nne ya mafunzo kwani ni mojawapo ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya Uwezeshaji.

"Hatua hii iliyofikiwa ni nzuri kwani itawawezesha wafanyabiashara wa Mkoa wa Geita kuweza kumudu mazingira na changamoto mbali mbali katika ushindani utakaokuwa unajitokeza katika Zabuni ambazo sio tuu za Mgodi wa Geita ila hadi sehemu nyingine." Aliongeza Katibu Mtendaji.

Katibu Mtendaji aliushukuru Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa kuwezesha Mradi huo kutekelezwa kwani Mgodi huo umekuwa mfano katika kushirikisha Wananchi kwenye miradi yake.

Katibu Mtendaji aliwaasa washiriki kuwa wafuatiliaji wazuri wa mafunzo lakini pia utekelezaji mzuri katika kongano watakazoanzisha.

Mwakilishi wa Mgodi wa Geita ambaye ndiye Mratibu kwa upande wa Geita Ndg. Reward Tenga aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Geita kwa Ushirikiano mzuri wanaouonesha katika mradi huo.

Alisema wafanyabiashara wengi wa Mkoa wa Geita ni wadogo hivyo kama wakianzisha Kongano itakuwa rahisi hata kufanya biashara sio tuu na Mgodi bali wakandarasi pia wa Mgodi huo wa dhahabu.

Alifurahishwa zaidi na wingi wa wafanyabiashara waliojitokeza kwenye mafunzo hayo na kusema kuwa ni mwendelezo mzuri wa Program hiyo.

Aliwaasa wafanyabiashara hao kutokufikiria tuu Mgodi wa Geita bali waangalie fursa nyingine zinazoweza kuwaongezea mtaji.

Pamoja na hayo mgeni rasmi alipata wasaa wa kutembelea kituo cha Uwezeshaji Mkoani Geita ambapo alijionea vifaa vipya vitakavyowasaidia Wananchi kupata taarifa na kutatua baadhi ya changamoto na kupata maelekezo ya msingi kutoka kwa watumishi wa Baraza na Taasisi nyingine zitakazokuwepo kituoni hapo.