Habari

Imewekwa: Feb, 11 2021

"​WANANCHI MKIKOPA MKUMBUKE KUREJESHA MIKOPO"

News Images

Hayo yalikuwa maneno ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim M. Majaliwa wakati akizindua maonesho ya nne ya Mifuko na Program za Uwezeshaji katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid Arusha.

Waziri Mkuu aliwataka Wananchi wote wanaonufaika na mikopo kutoka katika Mifuko ya Uwezeshaji kuhakikisha wanairejesha ili iweze kuleta tija na kuwanufaisha wengine.

Aidha Waziri Mkuu alisema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha inakuwa na Mifuko michache ila yenye kuleta tija.

Waziri Mkuu alitoa vyeti vya ushiriki kwa baadhi washiriki kwa makundi tofauti tofauti lakini pia alitoa mfano wa Hundi kwa vikundi na watu waliopatiwa mikopo na Mifuko.

Mfuko wa PASS TRUST ulitoa kiasi cha Shilingi milioni tisini pamoja na trekta la kulimia wakati mfuko wa SELF MICROFINANCE ulitoa mkopo wenye thamani ya zaidi ya milioni mia tatu.

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza Bibi. Beng'i Issa alisema kuwa maonesho ya mwaka huu yamekuwa tofauti na miaka miaka mingine.

"Katika maonesho ya mwanzo tumekuwa tukihusisha tuu Mifuko ya Uwezeshaji, baadaye tukavihusisha na vikoba. Kwa mwaka huu tumehusisha Taasisi za Fedha, Taasisi za Umma, Mashirika Binafsi, Taasisi za Bima na Wajasiriamali" alisema Katibu.

Aliongeza kuwa maonesho haya yatakuwa na faida kwa watu wa Kanda ya Kaskazini kwani wataenda kuitambua Mifuko mbali mbali kama inayotoa dhamana ya mikopo, inayotoa mikopo bila riba na mingineyo.

Uzinduzi huu ulihudhuriwa na Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro na Manyara na wakuu wa Taasisi mbali mbali za Umma na binafsi na Asasi za kiraia pamoja na kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Idd Kimanta.

Maonesho haya yalianza tarehe 7/02/2021 na yanatarajia kumalizika tarehe 13/02/2021 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama.