Habari

Imewekwa: Jun, 02 2021

WANAWAKE WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KATIKA BIASHARA ZAO ILI KUENDANA NA MABADILIKO.

News Images

Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng'i Issa wakati akizindua duka la mtandaoni la Wajasiriamali wa TASWE (Tanzania Saccos Women Entrepreneurs) katika hoteli ya Golden Tulip Dar es Salaam.

Katibu Mtendaji ameeleza kuwa ugonjwa wa korona umeleta athari kubwa kwa Wafanyabiashara ila wapo ambao wametumia janga hilo kama fursa na wamepata mafanikio makubwa Kiuchumi.

Alisema kuwa kwa kufanya biashara mtandaoni wanawake wanaweza kupata masoko hata nje ya nchi na kutanua wigo wa Biashara na Mitaji.

"Kwenye biashara ili ufanikiwe lazima uweke akiba na ukiweka akiba uwekeze ili iweze kuzalisha na isikae tuu, Tuweke Fedha zetu mahali ambapo ni salama na itazalisha na tufanye kazi zetu na kuendesha vikundi vyetu kwa mujibu wa sheria na taratibu." Aliongeza Katibu.

Alisema kuwa kwa muda sasa wanawake wamekuwa wakifanya biashara zao bila kutumia mitandao, hawarasimishi na hata wengine kuzifanyia majumbani. Ni muda muafaka sasa wa wao kubadilika na kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.

"Niwasihi Wafanyabiashara wanawake waanzishe tovuti, warasimishe biashara na kuongeza uzalishaji na tutumie sana Teknolojia" alisisitiza Katibu Mtendaji.

Alisema kuwa kwa sasa Serikali inashawishi wanawake wengi waweze kufungua makampuni lakini si hilo tuu imeenda mbele zaidi kwa kushirikiana na Taasisi ya PPRA kutoa mafunzo kwa wanawake ili waweze kujua taratibu za manunuzi za Serikali. Lengo kuu ni kuhakikisha angalau tunafikia asilimia 30 ya makampuni ya wanawake yanayofanya kazi na Serikali.

Nae Mwenyekiti wa TASWE Mama Anna Matinde, amesema kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikitoa mikopo na kuwatafutia masoko Wajasiriamali tangu ilipoanzishwa mwaka 2003.

Kwa namna ambavyo Teknolojia imebadilika wameona kuna haja sasa ya kuitumia mitandao ya kijamii na tovuti kukuza uchumi na Biashara. Na ndio maana wamekuja na wazo la kuanzisha duka la mtandaoni (taswestore.com) ambalo kila mwanachama wa TASWE ataweza kuonyesha na kuuza bidhaa zake.

Kutokana na hayo ndio maana Taasisi iliona kuna umuhimu wa kuandaa mafunzo kwa ajili ya wanachama wa TASWE ambao watafundishwa namna ya kutumia duka letu la mtandaoni kuuza bidhaa zao.

"Katika mafunzo haya ya siku nne, Wajasiriamali wanawake zaidi ya 100 watanufaika nayo na ni matumaini yetu kuwa wataondoka na kitu kukuza na kuinua uchumi wao binafsi na wa Taifa kwa ujumla." Alifafanua Mwenyekiti.