Uratibu wa Vikundi vya Kijamii

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi linahamasisha uanzishwaji na uimarishaji wa vikundi vy kiuchumi, hasa vikundi vya kifedha vya kiuchumi (Community Financial Group-CFG). Katika kutekeleza jukumu hili Baraza linashirikiana na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Sekta binafsi. Jitihada hizi zinalenga kukuza sekta isiyo rasmi ya kifedhanchini Tanzania na kuhakikisha inaratibiwa vizuri, watanzania wengi wananufaika na mchango wake katika uchumi wa Taifa unaweza kupimika kwa urahisi. CFG ni vikundi vinavyoanzishwa, kumilikiwa na kuongozwa na wanavikundi wenyewe kwa lengo la kujiwekea akiba na kukopeshana wenyewe kwa ajili ya kupata mitaji ya kufanya shughuli za kiuchumi. Vikundi hivi vinajumuisha vile vinavyoweka akiba na kukopeshana kwa njia ya mzunguko (ROSCAs), ASCAs, Vikundi vya VICOBA, VSLA, n.k.Hivi karibuni, CFG vimewavutia wawekezaji, watunga sera na wafadhili katika masuala ya huduma za kifedha kutokana na nafasi yake katika kuongeza wigo wa huduma jumuishi za kifedha Hata hivyo, pamoja na umuhimu wake katika kutoa huduma za kifedha katika jamii hasa wa kipato cha chini mijini na vijijini kuna changamoto mbalimbali katika mifumo hiyo. Changamoto hizo ni pamoja na:

  1. Kutokuwepo kwa taarifa na takwimu sahihi kuhusu CFGs na taasisi zinazosaidia uanzishwaji na uendelezaji wake;
  2. iKutokuwepo mfumo wa uratibu wa CFGs na taasisi wezeshi unaokidhi haja;

Baraza kwa kushirikiana na wadau husika wameweka utaratibu wa uratibu wa CFGs nchini Tanzania ambao utawezesha wadau kufahamu hali ya utekelezaji na mahitaji ya maboresho ambayo yatawezesha mfumo huo kufanya vizuri zaidi. Utaratibu huo unajumuisha ufanyaji wa mikutano ya mara kwa mara na wadau, hasa taasisi mwavuli kama VICOBA-FETA, TIMAP na IR VICOBA. Wadau wengine katika mikutano hiyo ni Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu ya Tanzania na FSDT. Lengo la mikutano hiyo ni kuimarisha uratibu na uendelezaji wa CFGs ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha na kuona kuwa watanzania wengi zaidi wanapata huduma za kifedha nchini. Jitihada hizi zinalenga katika kuhakikisha kwamba:

  1. Watanzania wengi zaidi wanajiunga na na kufaidika na CFGs kwa kujiwekea akiba na kupata mitaji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi;
  2. Kunakuwepo na mfumo imara wa uratibu wa CFGs kutoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa mpaka ngazi ya Taifa kuhakikisha kuwa taarifa na takwimu sahihi zinapatikana ya kupanga na kufanya maamuzi sahihi;
  3. Taasisi mwavuli au chombo cha kuunganisha CFGs kinaanzishwa katika ngazi ya Halmashauri za Mamlaka za Serikali za Mitaa;
  4. Mfumo rahisi wa TEHAMA kwa ajili ya CFGs (digital data collection) na kanzi data ya kitaifa ya CFGs na taasisi wezeshi unatengenezwa

Katika jitihada za kuwezesha maendeleo na uratibu wa CFGs yafuatayo yamefanyika:

  1. Mwongozo wa usajili na utoaji wa taarifa za CFGs uliandaliwa na kuanza kutumika tangu mwezi Oktoba 2016;
  2. Maafisa wa madawati ya Uwezeshaji katika ngazi za mikoa na Halmashauri walipatiwa mafunzo (ambao wanafanya kazi kwa ukaribu na Baraza) kuhusu matumizi ya mwongozo wa usajili na utoaji wa taarifa za CFGs pamoja na uanzishwaji na uendelezaji wa CFGs;
  3. Miongozo ya uanzishwaji wa CFGs ilipitiwa na kufanyiwa maboresho;
  4. Mwongozo wa kufundishia ujasiriamali kwa CFGs unaendelea kukamilishwa (Mwongozo unahusisha: mfumo wa ufundishaji ujasiriamali kwa CFGs; Mkakati wa utekelezaji wa mfumo wa kufundishia ujasiriamali kwa CFGs; na mpango kazi wa utekelezaji wa mfumo wa ufundishaji ujasiriamali kwa CFGs).
  5. Mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa CFGs uliandaliwa na unaendelea kutekelezwa.