Vituo vya Uwezeshaji

KITUO CHA UWEZESHAJI WANANCHI KAHAMA (KEEC)
1. Utangulizi

Kituo cha Uwezeshajini matokeo ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kasimu M. Majaliwa (Mb), ambaye alifanya ziara mkoani Shinyanga na baadae kwenye wilaya ya Kahama. Akiwa wilayani Kahama alitambua mchango wa uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga hususan Halmashuri ya Mji wa Kahama kwa kuchukua jitihada ya kutenga na kugawa maeneo ya kufanyia shughuli za uzalishaji kwa Wajasiriamali. Mhe. Waziri Mkuu alitembelea Halmashauri ya Mji wa Kahama na kubaini kuwa katika eneo la Bukondamoyo kumetengwa eneo la ekari 500 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogovidogo vya Wajasiriamali hasa vijana na wanawake. Katika eneo hilo viwanja 623 vimepimwa, kutolewa hati na kugawanywa kwa Wajasiriamali wazalishaji ili viwanja hivyo viweze kutumika kwa shughuli za uzalishaji na biashara nyingine ikiwemo kuweka mashine za kupasua mbao, useremala, uzalishaji, kuchomea vifaa mbalimbali (Welders), biashara za huduma na kufanya biashara ndogondogo.Aidha, katika eneo hilo Wajasiriamali 1,021 (wengi wao wakiwa ni vijana na wanawake) walipewa viwanja kulingana na shughuli wanazofanya.

Baada ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuona jitihada kubwa zilizofanyika wilayani Kahama, alitoa agizo kwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lianzishe Kituo Maalum cha kuhudumia wananchi kwenye masuala yote ya kiuchumi wakiwemo wajasiriamali, wakulima n.k. ambapo kituo hicho kinategemewa kuwa ni kituo cha mfano kwa Halmasahuri zote nchini.

Kituo cha Kahama kilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri MKuu (Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) mnamo tarehe 18 Novemba 2018. Kituo hichi kipo Kata ya Nyihogo, barabara ya Tabora.

2.Walengwa wa Kituo

Walengwa wa kituo ni wananchi na wajasiriamali wote wakiwemo wadogo, wakati na wakubwa, Vikundi na Makampuni yaliyopo katika Sekta zote za kiuchumi.

3.Umuhimu wa Kuanzisha Kituo

Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ni juhudi za makusudi zinazoanzishwa na Serikali ili kuwasaidia wananchi wake waweze kushiriki vizuri katika shughuli za kiuchumi. Uwezeshaji unaweza kufanyika kwa kupitia Sera sahihi, Sheria sahihi, kukuza ujuzi wa wananchi, upatikanaji wa mitaji nafuu, taarifa sahihi za masoko na programu mahsusi ambazo zinazompa fursa mwananchi ya kushiriki vizuri kwenye uchumi. Watanzania wengi sana wanahitaji kupata taarifa, elimu, ujuzi na mitaji ili kuweza kusonga mbele kwenye juhudi zao za kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Uanzishwaji wa kituo cha uwezeshaji ni utaratibu muafaka ambao utaondoa adha ya watanzania katika kutafuta taarifa, elimu na ujuzi kwenye maeneo ya biashara na mambo mengine ya kiuchumi, kufahamu taratibu za urasimishaji wa biashara, taarifa za masoko, kuongeza thamani ya mazao, kufahamu fursa za hifadhi ya jamii, kupata elimu ya kodi na kufahamu fursa za mitaji.

Kituo cha Uwezeshaji ni nyenzo muhimu ambayo itafanya baadhi ya Taasisi za Serikali za kitaifa ambazo zinatoa huduma mbalimbali kupata urahisi wa kuwafikia wananchi. Kabla ya kuanzishwa kwa kituo cha uwezeshaji wananchi hawata kuwa na mahala popote ambapo wanaweza kwenda kuuliza kama wana maswali yoyote. Vilevile kwa mwananchi ambaye hana taarifa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na serikali, akifika kituoni hapo ataelewa mambo mengi na huduma ambazo hapo awali alikuwa hazifahamu.

Kituo cha uwezeshaji ni tofauti na vituo vingine ambavyo vimewahi kuanzishwa, kwa sababu lengo lake kubwa ni kumwendeleza mwananchi kiuchumi kwa kuleta huduma zote za serikali na sekta binafsi katika eneo moja. Lakini pamoja na huduma hizo pia kituo kitamjengea uwezo mwananchi kielimu, kiujuzi, kitaarifa na kifedha. Hivyo inategemewa kwamba kituo kitaboresha huduma kwa wananchi pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi; na Kuongezeka kwa Ajira.

4.Madhumuni ya Kituo

Kituo cha Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi cha Kahamakimeanzishwa kwa madhumuni ya kutoa huduma kwa wajasirimali na wananchi kwa ujumla ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha ama kuendeleza biashara na miradi mbalimbali ya maendeleo. Madhumuni na majukumu ya kituo ni:-

a)Kutoa huduma za elimu na ujuzi mbalimbali

b)Huduma za kurasimisha biashara kama vile leseni na vibali vyote vinavyohitajika kama vile vibali vya shirika la viwango, mamlaka ya chakula na dawa, kurasimisha ardhi, huduma za msimbomilia

c)Huduma za kibenki na mikopo

d)Elimu ya kodi,

e)Elimu ya ufundi,

f)Elimu ya kuongeza thamani bidhaa,

g)Huduma za mikopo nafuu ya serikali kutoka kwenye mifuko ya serikali,

h)Huduma za bima ya afya,

i)Huduma za hifadhi ya jamii,

j)Elimu kwa ujumla,

k)Elimu ya vyama vya ushirika,

l)Elimu ya uanzishwaji wa vikundi vya kijamii n.k.

m) Kituo kitatoa huduma za maeneo ya kufanyia aina mbalimbali za biashara kutokana na ukubwa wa eneo la kituo na mazingira husika.

n)Huduma za masoko na kutengeneza mtandao wa masoko.

5.Taasisi zinazotoa Huduma Kituoni

Taasisi zinazotoa Hudumandani ya Kituo ni Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) Shirikisho la VICOBA Tanzania (VICOBA FETA), Taasisi ya VICOBA vya kidini (IR-VICOBA), Tanzania Informal Microfinance Association of Practioners (TIMAP), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Mfuko wa Pembejeo wa Taifa (AGITF), PASS TRUST FUND, Mpango Wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za wanyonge Tanzania (MKURABITA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), Mamlaka ya Uendelezaji wa Biashara (TANTRADE), SELF Microfinance Fund, GSI Tanzania Limited, Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), na Benki ya Taifa ya Biashara.

6.Utawala wa Kituo

Kituo hiki kinaratibiwana Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kahama.

Mwongozo wa Uendeshaji wa Kituo cha Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Kahama

Pakua Kipeperushi cha Kituo cha Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Kahama

Pakua Mwongozo wa Uendeshaji wa Vituo vya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi