Ufuatiliaji na Tathimini ya Uwezeshaji
Ufuatiliaji na Tathmini
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) linajukumu la kufuatatilia, kutathmini, kuandaa na kutoa taarifa za maendeleo ya shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi Tanzania Bara. Baraza linatekeleza jukumu hili kupitia katika kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini ambacho kinajukumu la kufuatilia utekelezaji wa programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi hapa nchini. Kitengo hiki kinatekeleza majukumu yake kwa kuandaa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini, kukusanya , kuchambua na kutafsiri takwimu mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha wataunga sera kutoa maamuzi sahihi kuhusiana na masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Mfumo wa ufuatiliaji na tahmini wa Baraza unawezesha wadau kushiriki katika ufuatiliaji na utoaji wa taarifa za shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi. Mfumo huu unaliwezesha Baraza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa programu na shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinazotekelezwa na wadau mbalimbali pamoja na kutoa taarifa za utekelezaji huo zikiwemo taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Baraza. Pia Mfumo huu unaliwezesha Baraza kutambua changamoto za utekelezaji na kuchukua hatua stahiki kwa wakati. Aidha, Mfumo huu unaliwezesha Baraza kutathmini utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NMSFEE) ambao unatoa mwongozo kwa wadau mbalimbali kuhusu jinsi ya kutekeleza programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi na kujifunza juu ya mbinu bora za kutekeleza programu hizo. Wadau wanaotekeleza Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni pamoja na taasisi za umma, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo.
Ufuatiliaji unafanyika kila siku na unahusisha ukusanyaji wa takwimu mara kwa mara, kuchambua na kutoa taarifa za matokeo ya tafiti hizo pamoja na tathmini za masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa uongozi wa Baraza, wadau wa maendeleo pamoja na wadau wengine. Ufuatiliaji unasaidia kupima utekelezaji wa malengo yaliyopangwa katika kipindi husika.
Kwa upande mwingine, tathmini inahusisha uchambuzi maalumu wa utekelezaji na matokeo ya utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi hapa nchini pamoja na mchango wa wadau mbalimbali katika utekelezaji wa Sera hiyo. Lengo la thathmini ni kujifunza na kupata uzoefu kutokana na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC Strategic Plan) pamoja na Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kichumi kwa ujumla. Thatmini inayofanywa na Baraza ni shirikishi ikiwawezesha wadau kushiriki kikamilifu katika tathmini za ndani na nje ambazo hufanyika katika kipindi maalumu kama vile kila baada ya miaka mitano.
Malengo ya kufanya tathmini ya Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi pamoja na Mpango Mkakati wa Baraza ni:
- Kupima ni kwa jinsi gani malengo yaliyowekwa kwenye Mkakati wa Baraza ni halisia na yanaweza kufikiwa/kutekelezwa;
- Kupima ni kwa jinsi gani utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Mpango Mkakati wa Baraza umetimiza malengo yake yaliyokusudiwa;
- Kupima ni kwa jinsi gani rasilimali (watu na fedha) za kutosha zinatengwa ili kuwezesha utekelezaji wa Sera na Mpango Mkakati wa Baraza;
- Kupima ni kwa jinsi gani Baraza linatumia rasilimali zilizopo katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi;
- Kupima na kutafiti sababu zinazochangia kufanikiwa au kutofanikiwa kwa utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi pamoja na Mpango Mkakati wa Baraza;
- Kupima matokeo na mabadiliko katika maisha ya wanawake, wanaume, vijana na watu wenye ulemavu nchini.
Utoaji waTaarifa
Taarifa za utekelezaji zinaandaliwa na kuwasilishwa kwa wadau husika kila baada ya miezi 3 na kila baada ya mwaka na wakati mwingine zinaandaliwa kulingana na mahitaji yanapojitokeza. Aidha, taarifa za utekelezaji wa Sera za mwaka zinaandaliwa na kuwasilishwa kwa wadau kila mwaka baada ya kukubaliwa na kupitishwa na uongozi wa Baraza.
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi linapenda kuwaomba wadau wote na watakelezaji wa mipango na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini kuandaa na kuwaasilisha taarifa zao za utekelezaji katika ofisi za Baraza kila baada ya miezi 3 na kila mwaka ili kuiwezesha Serikali pamoja na wadau wengine kuelewa ni kwa jinsi na kiwango gani sera, mipango na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi zimetekelezwa, nini changamoto za utekelezaji, mafanikio yaliyopatikana yakithibitishwa na hadithi/masimulizi ya mafanikio kutoka kwa walengwa pamoja na mambo ya kujifunza kutokana na utekelezaji uliofanyika.
Baraza linapenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wadau wote wa tafiti katika Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kutembelea ofisi zetu za Baraza kwa maelezo zaidi. Pia, wadau wengine wanaombwa kutembelea ofisi za Baraza pamoja na kuwasilisha hoja, michango na maswali kupitia barua pepe ifuatayo: neec@uwezeshaji.go.tz.