Programu

PROGRAM ZA BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI (NEEC)

1.0. KLINIKI YA UJASIRIAMALI KWA VIJANA WA ELIMU YA JUU

Inalenga vijana waliomaliza elimu ya juu au ambao bado wanasoma vyuoni. Inatekelezwa na Baraza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka sekta binafsi na umma na hufanyika kila mwaka tangu ilipoanzishwa mara ya kwanza mwaka 2013. Programu hii hutoa mafunzo ya wiki nane (8) ya ujasirimali na biashara yanayojumuisha pia mafunzo ya vitendo.Vijana huandaa michanganuo ya biashara na kushindanishwa. Baraza huwaunganisha na mitaji kwa kuwaleta pamoja wadhamini ambao hutoa zawadi za mbegu mtaji. Baraza hutoa huduma za ushauri katika kipindi cha uendeshaji biashara.

2.0.Kijana Jiajiri

Ni program ya Vijana wenye umri wa miaka 18-35. Inatekelezwa na Taasisi ya Ushindani na Ujasirimali nchini (TECC) ambayo imeanzishwa kwa ushirikiano kati ya Baraza, Taasisi ya Sekta Binafsi na Tume ya Sayansi na Teknolojia Nchini. Programu hii imejikita katika mafunzo ya wiki 6, mpango wa malezi na kuunganishwa na mitaji katika taasisi za fedha na mifuko ya uwezeshaji nchini.

3.0.JIANDALIE AJIRA (‘’VIA’’)

Hii ni programu mwendelezo ya Kijana Jiajiri ya kuendeleza Vijana inayoratibiwa na Taasisi ya Ushindani na Uendelezaji Ujasiriamali (TECC) iliyojikita katika kuwaandalia vijana ajira. Utekelezaji wa program hii unashirikisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Watoa Huduma za Uendelezaji Biashara chini ya Udhamini wa Taasisi ya Kimataifa ya Vijana (IYF). Programu hii imejikita katika Mafunzo ya Stadi za Biashara, Stadi za Kazi. TECC inashirikiana na IYF katika kutoa mafunzo ya wakufunzi kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa na SIDO kwa ajili ya kuwafundisha vijana katika maeneo mbalimbali nchini.

4.0.Ajira Yangu

Inalenga Vijana wenye umri wa miaka 18-35. Inatekelezwa kwa ushirikiano na ILO na Baraza. Programu hii Hutoa mafunzo ya ujasiriamali na biashara pamoja na malezi kwa vijana kwa muda wa miezi 2. Vijana huandaa michanganuo ya biashara ambayo hushindanishwa na washindi hupatiwa zawadi ya mbegu mtaji

5.0.Programu ya Vijana waendesha BODA BODA

Mpango unashawishi vijana kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa yaani SACCOS ili kujenga tabia ya kuweka akiba na kukopa. Lengo ni kuwa na SACCOS ya BODA BODA kila Mkoa nchini na kudhamini mikopo ya Boda Boda kupitia Mfuko wa Uwezeshaji. Programu hii inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Baraza na Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF). Katika program hii Vijana hupatiwa mafunzo ya ujasirimali, biashara, usalama na umuhimu wa hifadhi ya jamii.Mpaka sasa SACCOS 16 za Boda Boda zimeanzishwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Rukwa, Mara, Arusha, Mbeya, Dodoma, Ruvuma, Tanga na Geita.

6.0.Programu ya Vijana wa JKT

Inatekelezwa na Baraza kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika makambi yote nchini. Programu hii imejikita katika Mafunzo ya wiki 2 kwa wakufunzi na viongozi wa JKT ambapo mpaka Octoba 2016 mafunzo yametolewa kwa walimu wote wa JKT pamoja na viongozi wa kambi zote nchini. Lengo la programu hii ni kufikia vijana 7000 kila mwaka na itafanyika kwa miaka 5. Vijana wataunganishwa na taasisi za fedha kwa ajili ya kupata mikopo nafuu kwa kushirikiana na waratibu wa uwezeshaji katika Halmashauri zote nchini. Baraza litafuatilia maendeleo ya mafunzo ya ujasirimali katika kambi zote.

7.0 Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini chini ya Ofisi Waziri Mkuu.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu inatekeleza program ya kukuza Ujuzi Nchini ‘’National Skills Development Programme’’. Programu hii imekusudiwa kuwezesha nguvu kazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stakihiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Utekelezaji wa programu hii ni hatua za makusudi za Serikali za kukabiliana na kiwango kidogo cha ujuzi miongoni mwa nguvu kazi.

8.0 Programu ya SANVN Viwanda Scheme.

Ni mpango wa uendelezaji wa Viwanda vidogo na vya kati, unaoendeshwa na Taasisi tano shirika zikiwemo SIDO, BENKI YA AZANIA, NEEC, VETA na NSSF. Mpango huu unaoratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi unalenga kutatua changamoto ya ujuzi na mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs). Hii ni moja ya jitihada ya kuunga mkono sera ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wake Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambayo inalenga kuboresha maisha ya Watanzania kupitia Uchumi wa Viwanda.

9.0 Programu ya mafunzo kwa Wafanyabiashara wa Geita.

Programu hii imedhaminiwa na Mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML) na inaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Mafunzo haya yanalenga kuwapa ujuzi Wafanyabiashara wa Mkoa wa Geita, juu ya mchakato mzima wa kuwania zabuni zitolewazo na mgodi wa Geita Gold Mine. Programu hii inaunga mkono sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia ushirikiswaji wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini (Local Content).