Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC) limeendesha mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo Watoa huduma za Maendeleo ya Biashara, Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Maafisa Biashara kutoka halmashauri mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utekelezaji wa programu za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Mafunzo hayo yamewakutanisha washiriki kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Halmashauri ya Kilolo, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Halmashauri ya Mji wa Babati pamoja na Mji wa Gairo, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu namna bora ya kutoa huduma za maendeleo ya biashara na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC Bw. Gwakisa Bapala, alisisitiza umuhimu wa wataalamu hao kuwa chachu ya maendeleo kwa kuhakikisha elimu na huduma zinazotolewa zinafikia walengwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika jamii.
Aidha, Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Ushiriki wa Watanzania Bi. Neema Mwakatobe alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa NEEC wa kujenga mazingira wezeshi kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, huku akisisitiza matumizi ya maarifa na mbinu zinazolenga kuongeza tija katika biashara na miradi ya maendeleo.
Kwa upande wao, Wakufunzi wa Watoa huduma waliongoza vipindi vya mafunzo kwa kutoa maarifa kuhusu mbinu za utoaji huduma za maendeleo ya biashara, ushauri kwa wajasiriamali, pamoja na namna ya kuunganisha fursa za kiuchumi na mahitaji ya jamii katika maeneo yao ya kazi. Mafunzo hayo yaliwafikia zaidi ya walengwa 75.
NEEC imeendelea kusisitiza kuwa uwezeshaji wa kiuchumi unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Taasisi za serikali, wataalamu wa maendeleo na jamii ili kuhakikisha wananchi wanapata fursa stahiki za kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

