Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC) wameanza rasmi ziara ya kutembelea na kujifunza maendeleo ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki, maarufu kama East African Crude Oil Pipeline (EACOP), tarehe 20/04/2026. Ziara hii inalenga kutoa uelewa wa kina kuhusu mchango wa mradi huo katika kukuza uchumi wa taifa pamoja na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika fursa zinazotokana nao.
Msafara wa wajumbe bodi pamoja na Menejimenti ya NEEC umeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya NEEC, Profesa Aurelia Kokuletage Ngirwa Kamuzora, akishirikiana na Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Gwakisa Bapala, pamoja na timu ya menejimenti ya NEEC. Uongozi huo unahakikisha kuwa ziara hiyo inakuwa na tija kwa kuzingatia ajenda kuu ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa Watanzania kupitia miradi mikubwa ya kimkakati.
Katika ziara hiyo, wajumbe wanapata fursa ya kujionea kwa vitendo utekelezaji wa mradi huo na namna unavyotekelezwa kwa kuzingatia maslahi ya taifa. Mradi wa EACOP ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki, ukiwa na lengo la kusafirisha mafuta ghafi kutoka nchini Uganda hadi katika bandari ya Tanga nchini Tanzania. Kupitia mradi huu, fursa mbalimbali zimejitokeza kwa wananchi, ikiwemo ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, maendeleo ya ujuzi kupitia mafunzo, pamoja na ushiriki wa wazawa katika zabuni na manunuzi.
Moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika ziara hiyo ni tathmini ya ajira zilizotolewa kwa Watanzania. Wajumbe wanachunguza ni kwa kiwango gani wananchi wamenufaika na ajira hizo, ikiwa ni pamoja na ajira za muda mfupi na zile za kudumu, pamoja na mazingira ya kazi yanayotolewa. Aidha, wanazingatia namna mradi unavyochangia katika uhaulishaji wa teknolojia, ambapo wataalamu wa ndani wanapata nafasi ya kujifunza na kufanya kazi sambamba na wataalamu wa kimataifa.
Vilevile, ziara hiyo inalenga kuchunguza mchango wa mradi katika kukuza sekta ya ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kwa wazawa. Hii inahusisha ushiriki wa makampuni ya Kitanzania katika ugavi wa vifaa, huduma za usafirishaji, ujenzi na huduma nyingine zinazohitajika katika utekelezaji wa mradi. Kupitia hilo, NEEC inalenga kuhakikisha kuwa sera ya uwezeshaji wa wazawa inatekelezwa ipasavyo na kwa ufanisi.
Kwa upande wa jamii zinazozunguka mradi, wajumbe wanatazama namna ambavyo wananchi wanashirikishwa katika shughuli za maendeleo, pamoja na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha kuwa wanapata manufaa ya moja kwa moja. Hii ni pamoja na miradi ya kijamii kama vile elimu, afya, maji na miundombinu inayotekelezwa kama sehemu ya uwajibikaji wa kijamii wa mradi huo.
Ziara hiyo imeanza katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga, ambalo ni moja ya vituo muhimu vya mradi huo, na inatarajiwa kuhitimishwa katika wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Kwa ujumla, ziara hii ya NEEC ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati kama EACOP inaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa Taifa na wananchi wake. Kupitia tathmini hii ya moja kwa moja, Baraza linaweza kutoa mapendekezo yatakayoboreshwa zaidi utekelezaji wa miradi kama hii, na hivyo kuimarisha dhana ya uwezeshaji wa kiuchumi jumuishi nchini Tanzania

