
Katika kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikopo ya kuwezesha maendeleo ya viwanda nchini, Wajumbe wa Bodi ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na Menejimenti ya Sekretarieti ya NEEC wamefanya ziara ya kutembelea baadhi ya wanufaika wa mikopo inayotolewa kupitia mpango wa SANVIN Viwanda Scheme.
Ziara hiyo, inayofanyika tarehe 15-19 Julai 2025, inalenga kutathmini kwa vitendo namna mikopo hiyo imechangia katika kuendeleza shughuli za viwanda vidogo na vya kati, hususan kwa wajasiriamali wa Kitanzania wanaolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na maliasili nyingine kupitia uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani.
Wakiwa katika ziara hiyo, wajumbe walipata fursa ya kutembelea viwanda kadhaa vilivyoko katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Pwani, ambapo walishuhudia mafanikio ya moja kwa moja ya mikopo hiyo. Wanufaika walionesha mashine mpya walizonunua, kuongezeka kwa uzalishaji na hata ajira mpya walizozalisha kutokana na uwezeshaji huo wa kifedha.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya NEEC, Prof. Auleria Kamuzora, alisema:
"Tumeridhishwa na namna wanufaika wameweza kutumia mikopo hii kama kichocheo cha maendeleo ya viwanda vya ndani. Hii inaendana moja kwa moja na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha uchumi wa viwanda na kuwawezesha wananchi kiuchumi."
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC Bi. Neema Mwakatobe, alibainisha kuwa SANVIN VIWANDA SCHEME imekuwa nyenzo muhimu ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi zenye tija. Aliongeza kuwa Baraza linaendelea kutoa elimu, ufuatiliaji na msaada wa kiufundi kwa wanufaika wote ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kikamilifu na kwa matokeo yanayotarajiwa.
Kwa upande wao, baadhi ya wanufaika walitoa shukrani kwa NEEC na Serikali kwa kuwapa fursa ya kupata mikopo hiyo yenye masharti nafuu, wakisema imewasaidia kubadili maisha yao na kuongeza thamani ya biashara zao. Walisema bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu ya uendeshaji wa viwanda na masoko, wakihimiza NEEC kuendeleza juhudi hizo kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo.
Ziara hiyo imethibitisha kuwa uwezeshaji unaotolewa kupitia SANVIN Viwanda Scheme una mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa wajasiriamali wa ndani, huku NEEC ikiendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wake ili kufikia malengo ya maendeleo jumuishi na endelevu.