
BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limeendesha semina ya kuwajengea uwezo Waratibu wa madawati ya Uwezeshaji kwa ngazi za Wizara na Mikoa.
Semina hiyo ya siku mbili iliyofikia tamati leo imefanyika Mkoani Morogoro katika Hotel ya Edema huku ikifunguliwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji, Bibi Beng’i Issa.
Miongoni mwa waendesha mada waliofanikisha mafunzo hayo ni pamoja na Mkurugenzi wa Uwezeshaji na ushiriki wa Watanzania kaika Miradi ya kimkakati,Bi Neema Mwakatobe, Mkurugenzi wa huduma za Taasisi Bwana Gwakisa Bapala, Meneja wa uendelezaji wa biashara Bwana Siraji Nalikame na Meneja wa Mipango na Ufuatiliaji bwana Osward Karadisi.
Aidha katika semina hiyo kulikuwa na wawasilisha mada wengine kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu akiwemo Mkurugenzi wa Uwezeshaji na maendeleo ya sekta binafsi bwana Conrad Milinga na pia uwakilishi kutoka Mamlaka ya Serikali mtandao.
Wakati wa semina hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Bibi Beng’i Issa alisema kwamba lengo la semina hiyo ni kushirikishana uzoefu katika masuala ya Uwezeshaji ikiwemo ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati,matumizi ya vituo vya Uwezeshaji wananchi kiuchumi, fursa za mikopo ya asilimia kumi na program ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA).